11 wawania kuipeperusha bendera ya Chadema
17 Juni 2020Takriban siku 12 zilitolewa na chama cha Chadema kwa makada wake kuandika barua wakielezea kwa katibu mkuu wa chama hicho nia yao ya kuteuliwa na chama kwa lengo la kupeperusha bendera katika kinyang'anyiro cha urais ifikapo mwezi Oktoba, zimekamilika.
Kwa mujibu wa chama hicho, makada kindakindaki 11 wamejitokeza kila mmoja kwa wakati wake ndani ya muda uliowekwa, wakitekeleza kifungu cha kwanza cha muongozo wa chama wa kutangaza kusudio la kuwania nafasi za uongozi kwenye nafasi za uwakilishi serikalini.
Jina la mwendesha Bodaboda limekatwa kutoka kwenye orodha
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene amesema wanachama 11 pekee akiwemo mwanamke mmoja, Dokta Maryrose Majinge, ndio wamekidhi vigezo vya awali vya kutia nia kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Aidha, Makene ameongeza kusema kuwa jina la mwananchama mmoja ambae alipendekezwa na baadhi ya makundi ya vijana wanaofanya shughuli za bodaboda, limekatwa kutokana na kutozingatiwa kwa muongozo wa chama hicho katika kutia nia, hivyo kutoa sababu ya msingi kuliondoa jina hilo kwenye orodha ya waomba ridhaa.
Hii ni mara ya kwanza kwa idadi kubwa ya wanachama ndani ya chama hicho kujitokeza kuomba ridhaa akiwemo Freeman Mbowe mwenyekiti wa chama cha Chadema, Tundu Lisu, kaimu mwenyekiti wa chama hicho pamoja na Lazaro Nyalandu ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe ambao nao wameonesha kuwania nafasi hiyo ya juu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wachambuzi wanasema kunatarajiwa kushuhudiwa mchuano mkali kutokana na nguvu ya ushawishi wa kisiasa kwa makada hao ndani ya chama.
Takribana makada wote wa chama hicho walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya kukiwakilisha chama katika ngazi ya urais, waliweka nadhiri ya kuishughulikia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadhi ya sheria walizozitaja kandamizi endapo watafuzu kuteuliwa na chama chao kukiwakilisha.