1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

13 wauawa Nigeria

Charles Mwebeya17 Aprili 2007

Watu 13 wakiwemo Polisi wameuawa nchini Nigeria kufuatia ghasia za kisiasa nchini humo , wakati tume ya uchaguzi ikimuidhinisha Bwana Atiku Abubakar kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya Urais , katika uchaguzi wa jumamosi ijayo.

https://p.dw.com/p/CHG6

Polisi hao pamoja na mwanamke mmoja wameuawa kufuatia kundi la watu wasiojulikana kukivamia kituo kimoja cha Polisi cha Panshekara , katika jimbo la kaskazini ya nchi hiyo la Kano.

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo linalohusishwa na vuguvugu la kisiasa , amesema aliona kundi kubwa la watu wakiwemo wanawake wakielekea katika kituo kidogo cha Polisi mjini Kano leo mchana, ambapo walikivamia kituo hicho na kumpiga hadi kumuua Mkuu wa kituo hicho , mkewe, pamoja na askari wengine 11waliokuwa ndani ya kituo hicho.

Msemaji wa jeshi la Polisi mjini Abuja amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, na kusema ni askari watano tu waliofikwa na mauti katika ghasia hizo, ambazo amesema zimesababishwa na watu wenye imani kali za kidini.

Chanzo cha vurugu hizo bado hakijajulikana lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda kikahusiana na kitendo cha Polisi wa mjini Kano hivi karibuni kuwashambulia Raia waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa majimbo ambapo chama tawala cha PDP kiliongoza.

Jimbo la kaskazini la Kano ambalo linafuata sheria ya dini ya kiislam toka mwaka 2000, lina idadi kubwa ya wafuasi wa upinzani hususani vyama vya ANPP kinachoongozwa na Muhamad Buhari na Action Congress cha Atiku Abobakar.

Wakati huo huo tume ya uchaguzi nchini Nigeria imeridhia uamuzi wa mahakama kuu nchini humo kwa kumuidhinisha Bwana Atiku Abobakar kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi wa jumamosi ijayo.

Hatua hiyo imefuatia uamuzi wa mahakama kuu ya Nigeria hapo jana kumruhusu mgombea huyo wa chama cha Action Congress kuendelea na mbio za kuwania Urais, baada ya kuzuiliwa na tume ya uchaguzi hapo awali.

Atiku alizuiliwa na tume ya uchaguzi nchini Nigeria kugombea nafasi ya Urais kwa vile amefunguliwa mashtaka ya rushwa na tume ya makosa ya uchumi na fedha nchini humo .

Msemaji wa tume hiyo Philip Umeadi aliwaambia waandishi wa habari mjini Abuja kwamba Tume yake imewahakikishia Wanigeria wote kuwapo kwa jina la Atiku katika orodha ya wagom,bea watakaopigiwa kura siku ya Jumamosi.

Bwana Umeadi amesema taratibu zote kwa ajili ya uchaguzi huo zinaenda vizuri.

Kurejeshwa kwa jina la Atiku katika orodha ya Wagombea huenda kukasababisha ufinyu zaidi kwa upinzani kuchukua nafasi hiyo , kwani kama Atiku asingeruhusiwa kugombea , tumaini pekee kwa upinzani lingebaki kwa mgombea wa ANPP na mtawala wa zamani wa kijeshi wa nchi hiyo Muhamad Buhari.

Lakini wachambuzi wengine wa masuala ya kisiasa wanasema kumruhusu mgombea huyo wa Action Congress kugombea wakati zikiwa zimesalia siku tatu tu kufanyika uchaguzi huo ni ujanja uliofanywa na serikali ili kumdhibiti bwana Atiku dakika za mwisho.

Atiku Aboubakar wa AC na Muhamad Buhari wa chama cha ANPP ndio wagombea tishio dhidi ya mgombea wa chama tawala cha PDP, Umar Mussa Yaradua anayepigiwa upatu na Rais wa sasa Oleshegun Obasanjo.