1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

20 wauawa chuo kikuu Pakistan

Grace Patricia Kabogo20 Januari 2016

Zaidi ya watu 20 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Taliban katika chuo kikuu nchini Pakistan, huku Waziri Mkuu Nawaz Sharif akiapa kupambana na kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1HgOV
Gari la kijeshi la Pakistan likiingia kwenye Chuo Kikuu cha Bacha Khan baada ya mashambulizi ya Taliban.
Gari la kijeshi la Pakistan likiingia kwenye Chuo Kikuu cha Bacha Khan baada ya mashambulizi ya Taliban.Picha: Getty Images/AFP/A. Majeed

Idadi ya waliokufa imeongezeka kwa kasi baada ya watu wenye silaha kukishambulia chuo kikuu cha Bacha Khan mjini Charsadda, kilichopo umbali wa kilometa 50 kutoka mji wa Peshawar, katika shambulizi la hivi karibuni kwenye eneo hilo lililoathiriwa na mapigano.

Polisi, wanajeshi na vikosi maalumu walionekana kuingia katika eneo hilo kupitia ardhini na angani kwa lengo la kudhibiti shambuliz hilo, huku televisheni moja nchini humo ikiwaonyesha wanafunzi wa kike wakikimbia kuyaokoa maisha yao.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mkuu wa Polisi wa mkoa huo, Saeed Wazir amesema idadi ya vifo katika shambulizi hilo la kigaidi imefikia 21. Amesema shambulizi hilo lilisababisha kuwepo mapambano makali ya bunduki kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo wa Taliban, ambao wamekiri kuhusika na shambulizi hilo.

Imeelezwa kuwa operesheni imemalizika, huku wanafunzi wengi wakionekana kuwa wahanga waliouawa kwa kupigwa risasi katika bweni la wanafunzi wa kiume, katika chuo hicho kikuu kilichoko kwenye eneo ambalo ni ngome kuu ya wanamgambo wa Taliban. Zaidi ya watu 30 wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi na walinzi, wamejeruhiwa.

Washambuliaji wanne wauawa

Msemaji wa Jeshi, Meja Jenerali Asim Bajwa ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba washambuliaji wanne wameuawa. Hata hivyo bado haijafahamika iwapo washambuliaji hao wanne ni miongoni mwa watu 21 waliouawa. Taarifa za awali zilieleza kuwa watu sita wenye silaha walihusika katika shambulizi hilo.

Msemaji wa idara ya uokozi amesema idadi ya watu waliouawa inaweza ikaongezeka na kufikia 40 na miongoni mwa waliouawa ni wanafunzi, walinzi, askari polisi na profesa mmoja.

Gari la wagonjwa likiondoka kwenye eneo la tukio baada ya mashambulizi ya Taliban kwenye Chuo Kikuu cha Bacha Khan nchini Pakistan.
Gari la wagonjwa likiondoka kwenye eneo la tukio baada ya mashambulizi ya Taliban kwenye Chuo Kikuu cha Bacha Khan nchini Pakistan.Picha: Getty Images/AFP/A. Majeed

Kamanda wa Taliban Pakistan, Umar Mansoor amesema kuwa washambuliaji wake wanne waliojitoa muhanga ndiyo wamekishambulia chuo hicho kikuu. Mansoor amesema shambulizi hilo ni katika kujibu operesheni za kijeshi zinazofanywa dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali katika maeneo ya kikabila pamoja na kulipiza kisasi kutokana na wapiganaji wao kufa wakiwa mikononi mwa vikosi vya usalama vya Pakistan.

Afisa wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kiasi ya wanafunzi 1,000 walikuwa katika chuo hicho wakati ufyatuaji wa risasi ulipoanza. Taarifa ya jeshi imeeleza kuwa wanajeshi na askari polisi waliitwa kwenda kutoa msaada.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif amesema washambuliaji hao hawana imani yoyote wala dini na amelanii vikali shambulizi hilo. Katika taarifa yake, Sharif amesema serikali yake itaendelea na dhamira ya kuangamiza ugaidi nchini humo.

Shambulizi la leo linafuatia shambulizi jingine lililofanywa jana katika soko moja kwenye viunga vya mji wa Peshawar na kusababisha mauaji ya watu 10 akiwemo mtu aliyejitoa muhanga.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE, APE
Mhariri: Iddi Ssessanga