1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

50 WANUSURIKA NA AJALI YA NDEGE NIGERIA

23 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEFC

TAARIFA YA HABARI 23-10.05 17.00

LAGOS:

Kiasi cha abiria 50 wanatumainiwa wameokoka na ajali ya ndege iliotokea Nigeria.Wakuu wanawataka watumishi wote wa hospitali wanaomudu kuharakisha kwennda mkoa wa Oyo.Ndege chapa boeing 737 ilipakia watu 117 pale ilipotoweka jana usiku katika mitambo ya rada mara tu baada ya kuruka kutoka Lagos ikielekea mji mkuu Abuja.

Idadi kubwa ya wajumbe mashuhuri wa Nigeria ni miongoni mwa abiria.Miongoni mwa waliovuka salama na maisha ni makamo Katibu mkuu wa wa Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika magharibi (ECOWAS),Cheik Oumar Diarra wa Mali .

Jamadari Diarra ameweza kuwapigia simu jamaa zake mjini Bamako,Mali kuwaarifu kuwa amenusurika na maisha.

Hapo awali,msemaji wa serikali ya mkoa wa Oyo,kusini-magharibi mwa Nigeria ambako ndege hiyo iliangukia,aliarifu kwamba kiasi cha nusu ya abiria 117 waliokuwamo ndani ya ndege hiyo wamenusurika na maisha.Diop hakua na taarifa kuhusu wajumbe wengine wa Jumuiya ya ECOWAS waliokuwamo pia ndani ya ndege hiyo ya shirika la Belview.

CANCUN/MEXICO:

Kimbunga WILMA kinanyemelea sasa mkoa wa Florida,Marekani lakini dharuba na mvua kali imeendelea kuvuma katika mwambao wa pwani ya Karibik ya Mexico.

Wakuu wakijitahidi kuwapatia misaada maalfu ya watu walionaswa katika maeneo yao kutokana na dharuba ilioua si chini ya watu 8 hadi sasa.Mafuriko yamewafanya watalii kuparamia ghorofa za juu za mahoteli kujiokoa.

LONDON:

Waziri wa nje wa Marekani Bibi Condooliza Rice ameutaka UM leo hii kuichukulia Syria hatua kali akidai ripoti ya UM juu ya sehemu ya Syria iliochukua katika kuuwawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon,Rafik Hariri,haiwezi kuachwa juu ya meza tu.

Bibi Rice alikataa kuvumisha ni vikwazo gani UM huweza ukaichukulia Syria.Alisema tu ana uhakika jumuiya kimataifa ikijumuika pamoja itaamua nini la kufanya.

LONDON:

Marekani na Uingereza zimeshindwa katika juhudi zao za kupata imani za mamilioni ya wananchi wa Iraki .Mamilioni ya wairaki wanahalalisha hujuma za kujitoa mhanga kwa kujiripua dhidi ya majeshi ya muungano yaliopo Irak na hii inabainisha chuki zao dhidi ya kambi ya magharibi-ripoti ya vyombo vya habari imesema.

„45% ya wairaki wanaamini hujuma dhidi ya vikosi vya Marekani na Uingereza ni halali.82% wanapinga vikali kuwapo kwa vikosi vya kigeni nchini mwao-kwa muujibu wa gazeti la SUNDAY TELEGRAF lilivyoripoti hii leo likinukulu uchunguzi wa siri ulioamrishwa kufanywa na wizara ya ulinzi ya Uingereza.

KABUL:

Serikali ya Afghanistan leo imeitaka Marekani kumuadhibu yeyote yule ataekutikana na hatia ya kuhusika na kuchomwa moto kwa wafuasi wa kitalban nchini Afghanistan,kwani kitendo kama hicho kinatishia kuzusha hasira za wananchi dhidi ya majeshi ya kigeni yanayoikalia Afghanistan.

Msemaji wa wizara ya ulinzi jamadari Mohammed Zahir Azimi,amearifu kuwa serikali ya Afghanistan inachunguza tuhuma kuwa wanajeshi wa Marekani walizitia moto maiti za wapiganaji wa taliban na hivyo kukiuka desturi za kiislamu na sheria za kimataifa.

DUBAI:

Makamo wa kiongozi wa Al Qaeda, Ayman al-Zawahiri aliwataka leo waislamu wote kuwasaidia wahanga wa mtetemeko wa ardhi nchini Pakistan.Al –Zawahiri alitoa mwito huko ndani ya kanda ya video iliooneshwa na kituo cha TV cha Al-Jazeera.

Alinukuliwa kusema,

“Natoa mwito kwa waislamu wote kwa jumla na hasa jumuiya za misaada za kiislamu kuwapa ndugu zao wa kipakistan msaada tena haraka.”

Akaongeza kusema,

“Sote sisi tunajua vita dhaifu vya Marekani dhidi ya huduma za misaada zinazofanywa na waislamu.”-mwisho wa kumnukulu.

ASMARA:

Eritrea imekataa kuitikia mwito wa katibu mkuu wa UM Kofi Annan kuondoa marufuku ilioiwekea misafara ya ndege za helikopta ya vikosi vya kuhifadhi amani vya UM.Wajumbe wa kibalozi wamesema kwamba, rais Isaisas Affwerki alimuandikia katibu mkuu Annan akikataa kuondosha marufuku iliopigwa mwezi huu juu ya safari hizo.

Katibu mkuu Annan alimuandikia rais wa Eritrea, jumaane iliopita akielezea kuwa marufuku iliowekwa ni pingamizi kubwa kwa shughuli za vikosi hivyo vya UM mpakani mwa Ethiopia na Eritrea –vikosi vilivyowekwa huko tangu kumalizika kwa vita vilivyopita 2000 kati ya nchi hizi 2 jirani.

Eritrea mara kwa mara ikionya kuwa vita vipya vinafuka moshi kutokana na kubisha kwa Ethiopia kuidhinisha hukumu ya mwaka 2002 kuhusu wapi upite mpaka- iliotolewa na Mahkama ya kimataifa mjini The Hague.

BAGHDAD:

Waasi nchini Iraq wakishambulia kwa mabomu na kufyatua risasi kutoka motokaa wameua si chini ya watu 12 na kuwajeruhi si chini ya watu 12 pamoja na kuwajeruhi wengine kadhaa.Mtu aliejiripua kwa bomu kati kati ya mji wa Baghdad alizitekezea gari 2 za polisi na kuwaua askari 2 na raia 2.

Na huko kusini mwa Baghdad, bomu lililotegwa kando ya njia liliwajeruhi wairaki 2.Mabomu kadhaa pia yalilenga mlolongo wa magari ya Marekani na kuwaua si chini ya raia 2 na kuwajeruhi wengine 13.Wanajeshi 2 wa kimarekani wamejeruhiwa.

Na mjini Tikrit, bomu lililoegeshwa njiani lilimua askari polisi na watoto wake 4 waliokuwamo ndani ya gari pamoja nae.Na huko Baqouba,luteni-polisi ameuliwa kwa risasi zilizofyatuliwa kutoka gari lililokua likipita njia.

TEHERAN

Ndege kadhaa wanaoha eneo moja kuelekea jengine wanaanguka wakiwa wamefariki huko kaskazini-magharibi mwa Iran takriban kila siku-ripoti moja imesema.Hii imezusha zaidi hofu kuwa Iran karibuni itakuwa mojawapo ya nchi zilizoodhoreshwa na kesi za homa ya ndege ya mafua.

Shirika la habari la wanafunzi nchini Iran, ISNA limeripoti kuwa ndege 5,000 wamegunduliwa wamekufa magharibi mwa mkoa wa Azerbaijan unaopakana na Uturuki,Iraq na Jamhuri ya Azerbaijan.