Wabunge nchini Iraq wamchagua rais mpya
14 Oktoba 2022Licha ya makombora kadhaa kuvurumishwa Alhamisi kwenye majengo ya Bunge mjini Baghdad, wabunge hao wamemmchagua Rashid kuwa rais wa nchi hiyo na ambaye mara moja alimchagua Mohammed Shia al-Sudani, mwanasiasa wa Kishia kama waziri mkuu mteule.
Rashid alimtwika al- Sudani jukumu la kupatanisha makundi yanayohasimiana ya Kishia na kuunda serikali mwaka mzima baada ya Iraq kupiga kura mara ya mwisho. Sudani, ambaye anaungwa mkono na vikundi vyenye ushawishi vinavyoiunga mkono Iran, aliapa kuunda serikali haraka iwezekanavyo. Sudani amesema kuwa hawataruhusu hali ya kutengwa katika sera zao kwani tofauti zimeathiri taasisi za serikali ya nchi hiyo na kupoteza fursa nyingi za maendeleo.
Sudani anakabiliwa na changamoto
Lakini Sudani anakabiliwa na jukumu kubwa la kuwashawishi wapinzani wao ambao ni mamilioni ya wafuasi sugu wa mhubiri mashuhuri wa Kishia Muqtada al-Sadr.
Wakati huo huo serikali za Magharibi zimepongeza kwa haraka matokeo ya uchaguzi huo ambayo yanaleta matumaini ya kumaliza mzozo wa kisiasa wa Iraq.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa wito kwa viongozi hao wapya kuzingatia matakwa ya watu wa Iraq na kuzitaka pande zote kujiepusha na ghasia na kutatua tofauti kwa amani kupitia mchakato wa kisiasa. Ubalozi wa Ufaransa pia umempongeza Sudani kwa kuteuliwa kwake na kutoa wito wa kuundwa kwa serikali ambayo itafanya kila iwezalo kutimiza matakwa halali ya watu wote wa Iraqi na hasa vijana.
Shambulio lafanywa kuelekea bungeni
Siku ya Alhamisi wakati wabunge walikuwa wakilekea bungeni kwa mchakato huo wa uchaguzi, roketi tisa zilirushwa kuelekea katika eneo hilo. Duru ya usalama iliarifu shirika la habari la AFP kwamba takriban watu 10 walijeruhiwa ikiwa ni pamoja na maafisa sita wa vikosi vya ulinzi ama walinzi wa wabunge hao pamoja na raia wanne katika wilaya ya karibu.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, balozi wa Marekani Alina Romanowski alilaani shambulizi hilo kwa maneno makali na kuonya kwamba watu wa Iraq lazima watatue tofauti zao za kisiasa na malalamiko kwa njia za amani pekee. Aliongeza kwamba mashambulizi kama hayo yanadhoofisha demokrasia na kuiweka Iraq katika hatari ya vurugu za kila mara.