1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABIDJAN : Kikosi cha Morocco chazuliwa kambini

22 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBgP

Umoja wa Mataifa unachunguza madai ya dhuluma na unyonyaji wa ngono uliotapakaa unaofanywa na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast.

Umoja wa Mataifa umesema kikosi cha wanajeshi 800 wa Morocco miongoni mwa vikosi vyake vilioko Bouake ngome kuu ya waasi huko kaskazini kimezuliwa kambini.

Madai ya dhuluma za ngono yamekuwa yakitolewa mara kadhaa dhidi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa katika shughuli zao za kulinda amani na kupelekea Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kutangaza sera ya kutovumiliwa kabisa kwa vitendo hivyo.

Jean-Marie Guehenno Mkuu wa masuala ya kulinda amani wa Umoja wa Mataifa anasema ni muhimu sana kuhakikisha kwamba vikosi vinapata ujumbe huo na kila panapotokea jambo la aina hiyo wanajeshi hurudishwa nyumbani na nchi wanachama huchukua hatua za nidhamu.

Annan kabla ya kung’gatuka kwake hapo mwezi wa Desemba mwaka 2006 alisema unyonyaji wa ngono na dhuluma za ngono ni mambo yasiokuwa na uadilifu kabisa na hayakubaliki na shughuli za Umoja wa Mataifa na kwamba vitendo hivyo vitachukuliwa hatua za adhabu.