Wafanyakazi wa treni na viwanja vya ndege wagoma Ujerumani
7 Machi 2024Wafanyakazi wa reli na viwanja vya ndege nchini Ujerumani, wameanza mgomo mkubwa leo kushinikiza nyongeza ya mishahara.
Ujerumani imekabiliwa na migomo kwa miezi kadhaa sasa, huku wafanyakazi na uongozi wakishindana juu ya madai hayo, katikati mwa mfumuko mkubwa wa bei na kuyumba kwa biashara.
Wafanyakazi wa reli walianza mgomo wa masaa 35 katika treni za mizigo tangu jana Jumatano, huku mgomo wa treni za abiria ukianza leo asubuhi. Chama cha madereva wa treni cha GDL kinashinikiza kupunguzwa masaa ya kazi kwa wiki kutoka masaa 38 hadi 35.
Shirika la reli la Deutsche Bahn limelaani mgomo huo, likisema limefanya makubaliano ya nyongeza ya asilimia 13 ya mishahara. Wakati huo huo, wafanyakazi wa shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa, nao watafanya mgomo wa nchi nzima kuanzia leo.