1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Abiria wahangaishwa katika uwanja wa ndege Uganda

Lubega Emmanuel 17 Novemba 2023

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameagiza idara ya intelijensia ya jeshi kuwaondoa mara moja maafisa wake kutoka uwanja wa kimataifa wa ndege wa Entebbe, bila ya kutoa sababu ya agizo lake.

https://p.dw.com/p/4Z2pS
Uganda Kampala | Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: SNA/IMAGO

Kwa muda mrefu, wasafiri wa kigeni na pia raia wa Uganda wametoa vilio kuhusu mienendo ya kutozwa pesa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe wanapowasili au kuondoka. Baadhi wameweza kunasa kwenye video matukio hayo na kuyasambaza kwenye mitandao ya kijamii kama ushahidi.

Mamlaka ya usimamizi wa ndege - UCCA ilijibu vilio hivyo kwa kubadilisha utaratibu wa kuwashughulikia wasafiri kuwa waziwazi ili pasitokee fursa kwa mtumishi yeyote kuwanyanyasa wasafiri kwani hii imekuwa sifa mbaya kwenye uwanja huo.

Uganda yakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa Congo

Lakini mamlaka hiyo imekuwa ikikabiliwa na wakati mgumu kuwadhibiti maafisa wa idara ya intelijensia ya jeshi la nchi maarufu kama CMI ambao wamedaiwa kuendelea kuwanyanyasa wasafiri na watu wengine kwenye uwanja huo. Huenda sasa suluhu limepatikana baada ya rais Museveni mwenyewe kuagiza maafisa hao wa CMI kuondoka mara moja kwenye uwanja huo akihoji kuwa haoni wanachokifanya sehemu hiyo.

Agizo hilo linajiri siku mbili kabla ya Uganda kuwa mwenyeji wa kongamano la shirikisho la mashirika na makampuni ya ndege litakalowaleta pamoja wajumbe zaidi ya 500 kutoka mataifa 40. Baadhi ya raia wamelezea kuwa angalau rais anashughulikia jambo ambalo mashirika hayo yangetarajiwa kutaka ufafanuzi kwenye kongamano hilo.

Lubega EmmanuelDW Kampala.