1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy akabiliwa na changamoto kubwa Ethiopia

25 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyeshinda tuzo ya Nobel Abiy Ahmed anakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika uongozi wake wakati ambapo maafisa wanasema huenda ikawa makumi ya watu wamefariki dunia.

https://p.dw.com/p/3Rx9n
Russland | Afrika Gipfel in Sotschi
Picha: picture-alliance/dpa/Bildfunk/Kremlin

Haya yamejiri katika siku mbili za machafuko yaliyosababishwa na mzozo kati ya maafisa wa usalama nchini humo na mwanaharakti mmoja maarufu.

Wiki mbili hazijakwisha sasa tangu Abiy atunukiwe tuzo ya amani ya Nobel kutokana na mabadiliko aliyoyafanya yakiwemo kumrudisha nyumbani kutoka uhamishoni mwanaharakati Mohamed Jawar na wakosoaji wengine wa serikali pamoja na wanasiasa wa upinzani, ambao walikuwa wanachukuliwa kama magaidi na utawala uliopita.

Äthiopien Diskussion Medien und Demokratie in Addis Abeba | Jawar Mohammed
Mwanaharakati Mohamed JawarPicha: DW/Y. Gebregziabher

Huenda Jawar akawania uongozi katika uchaguzi wa mwakani

Lakini wiki hii, Jawar ambaye ni mjasiriamali wa vyombo vya habari ambaye wengi wanasema alikuwa na mchango mkubwa katika kuachia ngazi kwa waziri mkuu wa uongozi uliopita licha ya kuwa hakuwepo nchini humo, alisema polisi waliizunguka nyumba yake na kujaribu kuwaondoa maafisa wa usalama waliokuwa wanamlinda. Hilo ndilo jambo lililozua maandamano katika Mji Mkuu Addis Ababa na miji mingine na kupelekea vifo vya watu kumi na sita na wengine wengi kujeruhiwa.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Jawar, amedokeza kuwa huenda akawania uongozi katika uchaguzi wa mwakani, ingawa ameonya pia kwamba kuandaa uchaguzi katika hali iliyoko sasa ni jambo la hatari kwa Ethiopia.

"Najua Waziri Mkuu anataka uchaguzi ufanyike sasa, najua wengi katika upinzani wanataka uchaguzi ufanyike kwa haraka sasa hivi, makundi mawili moja la Waziri Mkuu na moja la upinzani ambao wana uhakika kwamba watashinda. Ndio unaweza kushinda, ingawa unaweza kushinda uchaguzi na uipoteze nchi. Nafikiri watu wanastahili kuwa makini sana kuanza sasa kwenda mbele," alisema Jawar.

Uchaguzi wa mwakani utakuwa mtihani mkubwa kwa Waziri Mkuu Abiy

Matamashi haya ya Jawar ndiyo ukosoaji mkubwa kabisa wa mwanaharakati huyo kwa Waziri Mkuu Abiy kufikia sasa. Wawili hawa walikuwa marafiki wakubwa ingawa mgawanyiko huu unafuatia kauli aliyoitoa Abiy bungeni mapema wiki hii, akionekana kumuelekezea Jawar ambaye ni Muethiopia ila ana pasipoti ya Marekani. Abiy alisema, "wamiliki wa vyombo vya habari ambao hawana pasi za kusafiria za Ethiopia wanacheza pande mbili, iwapo jambo hili litauendea kinyume usalama wa Ethiopia basi tutachukua hatua."

Unterstützer von Jawar Mohammed versammeln sich in Addis Abeba
Wafuasi wa Mohamed Jawar wakiandamana EthiopiaPicha: AFP/Stringer

Iwapo uchaguzi wa mwakani utakuwa huru na haki kama alivyoahidi Abiy, itakuwa ni kama mtihani kwa Waziri Mkuu huyo kijana iwapo anaweza kulileta pamoja taifa hilo lenye idadi ya watu milioni mia moja ambalo limegawika.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema tangu Abiy aingie madarakani, kumekuwa na wimbi la kamatakamata ya watu wanaoaminika kuwa wapinzani wa serikali katika eneo la Oromiya.