ABUJA : Mkutano wa OPEC wafanyika Nigeria
14 Desemba 2006Umoja wa Nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC unakutana mjini Abuja Nigeria leo hii kupanga sera ya uzalishaji wa mafuta katika kipindi cha majira ya baridi ukiwa chini ya shinikizo kutoka mataifa yanayoagiza mafuta duniani kuepukana na upunguzaji zaidi wa kiwango cha uzalishaji mafuta kunakohatarisha kupanda kwa bei ya mafuta na kuathiri ukuaji wa uchumi.
Umoja huo ambao huzalisha zaidi ya theluthi moja ya mafuta duniani tayari umepunguza kiwango cha uzalishaji mara moja mwaka huu kwa mapipa milioni moja na laki mbili kwa siku au asilimia nne hapo mwezi wa Oktoba ili kuzuwiya kushuka kwa bei hiyo kwa wiki 10 kwa asilimia 25.
Hivi karibuni kabisa kulikuwa na hisia nzito kwamba upunguzaji zaidi wa uzalishaji wa mafuta utaidhinishwa huko Abuja lakini kutokana na mashaka makubwa ya mataifa yanayoagiza mafuta mwelekeo huo inaonekana kubadilika.