1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABUJA: Waangalizi wa Umoja wa Ulaya waukososa uchaguzi wa Nigeria

24 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7Z

Waangalizi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na waangalizi wengine wamekosoa vikali jinsi uchaguzi wa Nigeria ulivyofanyika. Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Max van den Berg, amesema katika taarifa yake kwamba uchaguzi huo haukuwa halali.

Umaru Yar Adua wa chama tawala cha Peoples Democtaratic alitangazwa kuwa rais mpya wa Nigeria hapo jana. Matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo yalimpa gavana huyo wa jimbo la Katsina, kaskzaini mwa Nigeria, kura milioni 24. Mpinzani wake wa karibu alipata kura milioni sita pekee.

Msemaji wa upinzani nchini Nigeria, Tom Ikmi, amesema chama chake na vyama vyengine vitawasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Rais mteule, Umaru Yar Adua, ameutetea uchaguzi wa Nigeria akisema ndio mzuri kuwahi kufanyika nchini humo.

´Watu wana maoni yao tofauti. Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake. Watu wengine wanaamini huu ni uchaguzi mzuri zaidi kuwahi kufanyika nchini humu.´

Rais anayeondoka, Olusegun Obasanjo, amekiri uchaguzi wa Nigeria ulikabiliwa na mizengwe. Ametoa mwito makosa yote yyarekebishwe kabla tarehe 29 mwezi ujao wakati anapotakiwa kisheria kuondoka madarakani.

Watu takriban 200 nchini Nigeria waliuwawa katika kipindi cha wiki moja iliyopita kwenye machafuko yaliyozuka kuhusiana na uchaguzi.