1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abuja:Mgombea Urais Nigeria asafirishwa kwa matibabu Ujerumani

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLX

Mgombea Urais kwa tiketi ya chama tawala cha Peoples Democratic nchini Nigeria YarÁdua, amesafirishwa hadi Ujerumani kwa matibabu. Bw Umaru Yar´Adua mwenye umri wa miaka 55 na gavana wa jimbo la kaskazini la Katsina, amekua zingatio la vyombo vya habari nchini Nigeria , kuhusiana na afya yake, tangu alipoteuliwa kuwa mgombea Urais wa chama tawala mwezi Desemba. Jumatatu wiki hii alishindwa kufika katika mkutano mkubwa wa hadhara wa kampeni ya uchaguzi mjini Lagos.

Bw YarÁradua alipelekwa hospitali mjini Abuja Jumatatu kabla ya kusafirishwa hadi Ujerumani alikowasili leo asubuhi. Hakujatolewa maelezo zaidi juu ya kile anachougua, lakini amekua akisumbuliwa na figo. Uchaguzi wa rais nchini Nigeria umepangwa kufanyika mwezi Aprili kumchagua atakayeshika nafasi itakayoachwa na Rais wa sasa Olusegun Obasanjo, ambaye kwa mujibu wa katiba hatoweza kugombea tena, baada ya kumaliza mihula miwili ya miaka mine kila mmoja.