ABUJA:Ujumbe wa ECOWAS kutathmini maandalizi ya uchaguzi Nigeria
1 Februari 2007Ujumbe Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS unatarajiwa nchini Nigeria hii leo kutathmini maandalizi ya uchaguzi wa urais na wabunge uliopangwa kufanyika mwezi Aprili.
Ujumbe huo unaongozwa na Rais wa zamani wa Gambia Dauda Jawara vilevile kujumisha wajumbe wawili wa baraza la viongozi wa Jumuiya hiyo inayoshirikisha mataifa 15 ya Afrika Magharibi.
Kundi hilo la viongozi linatarajiwa kukutana na washika dau wote katika uchaguzi huo mkuu wakiwemo waandishi wa habari na wanachama wa mashirika ya kisheria.
Utafiti wa tathmini hiyo utakabidhiwa kiongozi wa Halmashauri ya Jumuiya ya Ecowas ili kuiwezesha kujua misaada vilevile ujumbe wa waangalizi watakaohitajika katika shughuli hiyo.
Nchi ya Nigeria ni moja ya mataifa waanzilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS iliyoanzishwa mwaka 75 kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi,amani na ustawi katika eneo hilo.