1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ACCRA: Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika kumalizika leo

3 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBmQ

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika unamalizika leo mjini Accra Ghana.

Tofauti kubwa zilidhihirika jana kwenye mkutano huo kuhusu kuunda muungano wa Afrika huku baadhi ya viongozi wakiwashauri wenzao wasiharakishe uamuzi huo na badala yake kutaka wazingatie maingiliano ya kikanda.

Viongozi wa serikali walikutana faraghani jana kwa mazungumzo yaliyotuwama juu ya kuunda nchi moja ya Afrika au kuboresha taasisi zilizopo.

Rais Muamar Gadafi wa Libya amekuwa akisisitiza kuundwe umoja wa Afrika utakaokuwa na serikali itakayochukua nafasi ya halmashauri ya sasa ya Umoja wa Afrika, kuunda sera moja ya kigeni na ulinzi na kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Lakini viongozi wengine akiwemo rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Umaru Yar´Adua wa Nigeria, wanataka Umoja wa Afrika upewe muda ukomae.

Rais Yar Adua amesema anaunga mkono ushirikiano ya kisiasa na kiuchumi ambao hatimaye utapelekea kuundwa kwa serikali moja ya nchi za Afrika.