1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adesina ni rais mpya wa Benki ya Afrika ya Maendeleo

29 Mei 2015

Benki ya Afrika ya Maendeleo, ADB imepata rais mpya, waziri wa kilimo wa Nigeria Akinwumi Adesina, ambaye amewashinda wapinzani 7 katika duru 6 za uchaguzi. Anachukua nafasi ya Donald Kaberuka anayemaliza muda wake.

https://p.dw.com/p/1FYaV
Akinwumi Adesina, rais mteule wa Benki ya Afrika ya Maendeleo, ADB.
Akinwumi Adesina, rais mteule wa Benki ya Afrika ya Maendeleo, ADB.Picha: DW/T. Mösch

Akinwumi Adesina aliibuka mshindi baada ya duru sita za uchaguzi, zilizomalizika jana jioni katika makao makuu ya Benki ya Afrika ya Maendeleo mjini Abidjan, Cote d'Ivoire. Adesina, msomi mwenye shahada ya uzamili katika masuala ya uchumi na maendeleo, anachukua hatamu za benki hiyo ambayo inajikuta katika mazingira mapya kifedha barani Afrika.

Baada ya kupata ushindi wa karibu asilimia 60 ya wajumbe wa bodi ya magavana wa benki hiyo, Akinwumi Adesina alisema atakuwa rais mwenye kujituma.

''Nataka kuwahakikishia, kwamba kama rais wa benki hii, nitakuwa rais mwenye kuwajibika, mwenye bidii, na mwenye mwelekeo. Nitakuwa rais atakayefanya kazi pamoja nanyi, katika hali ya ushirikiano, kujengea kwenye msingi mzuri kabisa unaoachwa na rais Kaberuka''. Amesema Adesina.

Mrithi mwenye uwezo

Rais wa sasa wa benki hiyo ambaye muda wake utamalizika tarehe 1 Septemba, raia wa Rwanda Donald Kaberuka, katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, amesema ana uhakika kwamba mrithi wake ataweza kuipeleka Benki ya Afrika ya Mendeleo kwenye hatua mpya ya maendeleo.

Donald Kaberuka, rais wa ADB anayemaliza muda wake
Donald Kaberuka, rais wa ADB anayemaliza muda wakePicha: Getty Images/C. Somodevilla

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo alimwambia rais mteule, Adesina kwamba jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kwamba benki hiyo am.bayo imefanya vyema mnamo miaka 10 iliyopita, kuweza kufanya yale ambayo benki za biashara haziwezi kuyafanya.

Benki hiyo inakabiliana na changamoto ya mazingira mapya kifedha, hususan kwa sababu nchi nyingi za kiafrika hivi karibuni zimekuwa zikitafuta fedha kwa wakopeshaji wapya, hasa China, na nyingine zimeanza kufuata njia mpya ya kujipatia fedha kwa kuuza dhamana za serikali.

Changamoto nyingine iliyopo ni mgawanyiko wa maoni ya wadau wa benki hiyo, juu ya iwapo inapaswa kujikita katika kuvutia mitaji ya watu binafsi katika ujenzi wa miundombinu, au ikiwa ni bora kuingia katika sekta mpya, kama vile kuzisaidia nchi maskini wanachama kupata mikopo kutoka katika masoko ya kimataifa.

Benki katika hali ya kuvutia

Kwa sasa Benki ya Afrika ya Maendeleo inao uwezo wa kugharimia sehemu ndogo tu ya maombi ya mikopo, lakini siku za hivi karibuni imekuwa ikitumiwa kiwango chake cha ukopaji chenye hadi murua ya AAA, kuvutia uwekezaji binafsi katika miradi barani Afrika.

ADB inagharimia miradi mingi ya maendeleo barani Afrika
ADB inagharimia miradi mingi ya maendeleo barani AfrikaPicha: AfDB/Jaques Fernandes

Rais mpya, Akinwumi Adesina ambaye alichaguliwa na jarida la Forbes kama mtu wa mwaka wa Afrika mwaka 2013, amepata sifa ya kufufua kilimo nchini Nigeria, ambacho kilikuwa katika hali ya kupuuzwa alipoteuliwa waziri wa kilimo mwaka 2011. Katika muda wake kwenye wizara hiyo mazao ya kilimo yameongezeka kwa tani milioni 22, hali ambayo imepunguza kwa zaidi ya theluthi moja kiwango cha chakula ambacho Nigeria inakiagiza kutoka nje.

Hali kadhalika, kulingana na taarifa za serikali ya Nigeria, sekta ya kilimo imeweza kuunda nafasi milioni tatu za ajira mnamo kipindi hicho.

Kuchaguliwa kwake kumekiuka kanuni zisizo rasmi za benki hiyo, kuwa rais wa nchi hiyo anatoka katika nchi ndogo wanachama, au za tabaka la kati. Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa zaidi wa watu barani Afrika, ambayo pia inaongoza kwa uchumi mkubwa barani humo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo