AFCON 2013: Macho yote kwa Cape Verde
2 Februari 2013Wakaazi hao wa visiwani wanapambana na vigogo wa soka barani Afrika Ghana katika mchezo mwingine leo wa robo fainali mwanzoni mwa awamu ya mtoano katika fainali hizi za 29 mwaka huu.
Cape Verde, ikiwa na idadi ya wakaazi wapatao zaidi ya nusu milioni tu na kundi dogo la wachezaji ambao wanaweza kuitwa kucheza timu ya taifa , wamewaacha mashabiki wa soka midomo wazi na kunyakua nafasi miongoni mwa timu nane bora katika bara la Afrika , katika mara yao ya kwanza kushiriki katika mashindano haya makubwa katika bara la Afrika.
Ushindi wa kushangaza dhidi ya Angola katika mchezo wao wa mwisho katika kinyang'anyiro cha makundi , kufuatia sare mara mbili, umewafanya wakaazi hao wa visiwani kuwa kionjo maridadi kwa wapenzi wa soka duniani kote.
Cape Verde ghafla imetoka kutoka timu ngeni katika mashindano haya na kuepuka kuaibishwa na kuwa timu ambayo inaamini kuwa inaweza kufikia nusu fainali.
Cape Verde kunyakua kombe?
"Hii ni timu yenye kujiamini na tumezidi sasa kujiamini tangu mashindano haya yaanze. Tuna uwezo, " amesema kocha Lucio Antunes.
Ghana wana mchezaji Mubarak Wakaso, ambaye amefunga bao pekee wakati walipoishinda Cape Verde katika mchezo wa kirafiki nchini Ureno mwezi Novemba, ambaye anarejea uwanjani mjini Port Elizabeth baada ya kukaa nje kutokana na kadi nyekundu.
Mpambano huo unafuatiwa na mpambano baina ya wenyeji wa mashindano Afrika kusini maarufu kama Bafana Bafana mjini Durban dhidi ya Mali , timu ambayo imemaliza ikiwa yatatu katika kinyang'anyiro cha mwaka jana.
"Kucheza na wenyeji wa mashindano na mashabiki wao wakiwa nyuma yao ni hadhi kubwa na changamoto kubwa , tunashauku na tunalisubiri kwa hamu pambano hili, amesema kocha Patrice Carteron.
Bundesliga
Na katika bundesliga, Nils Petersen alipachika mabao mawili katika mpambano wa duru ya 20 katika bundesliga na kuipa Werder Bremen ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hannover 96, ikiwa ni ushindi wa kwanza wa Bremen katika mwaka huu jana Ijumaa.
Bremen walitengeneza nafasi kadhaa za kufunga kabla ya Petersen hatimaye kuvunja ukame wa magoli kwa timu hiyo katika dakika ya 85, wakati Eljero Elia alipowatoka walinzi wawili wa Hannover na kummegea pande mfungaji.
Bremen ilitengeneza nafasi 32 za kufunga ikilinganishwa na sita za Hannover . Kocha wa Bremen Thomas Schaaf amesema kuwa, ingekuwa maafa makubwa iwapo tusingetumia nafasi tulizozipata. Ushindi huo unaiinua Bremen hadi nafasi ya 11, point moja nyuma ya Hannover, kabla ya michezo mingine hii leo na kesho.
Leo (02.02.2013) Fortuna Dusseldorf inaikaribisha VFB Stuttgat, Mainz ina kibarua na viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich, Hoffenheim inaikaribisha nyumbani Freiburg, wakati Schalke 04 iko nyumbani ikiwakaribisha Greuther Fuerth. VFL Wolfsburg ina miadi na FC Augsburg, wakati Eintracht Frankfurt inasafiri hadi mjini Hamburg kupambana na klabu ya mjini humo.
Kesho Jumapili (03.02.2013) itakuwa ni zamu ya mabingwa watetezi Borussia Dortmund ambayo itakuwa na mpambano wa kuamua nani hasa anashika nafasi ya pili wiki hii kati yake na Bayer Leverkusen. Leverkusen inashikilia nafasi ya pili hadi sasa na Dortmund inashikilia nafasi ya tatu, timu hizo zinapishana kwa point moja. Nuremberg ina miadi na Borussia Moenchengladbach.
Liverpool na Manchester City
Wakati huo huo Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amewaonya wachezaji wake kuwa Liverpool ina uwezo wa kutoa pigo jingine katika matumaini yao ya kuwania taji la msimu huu katika mpambano wao kesho Jumapili(03.02. 2013).
Mabingwa hao watetezi wa Premier League wamepoteza nafasi ya kutoa mbinyo kwa viongozi wa ligi ya msimu huu Manchester United wakati walipolazimishwa sare ya bila kufungana na QPR katikati ya wiki na wanaweza kurudi nyuma hadi kupishana na Manchester United kwa points kumi wakati watakapokumbana na Liverpool kesho.
Iwapo United itaishinda Fulham leo , utetezi wa City wa taji lake utakuwa katika hatari kubwa na Mancini anatambua fika kuwa Liverpool ina vipaji ambavyo vinaweza kuongeza matatizo kwa timu yake.
Mancini pia ana matumaini kuwa miezi ya Februari na Machi ambayo United itakuwa na michezo mingi na migumu ambapo itakumbana na Real Madrid katika kinyang'anyiro cha Champions League cha timu 16 zilizobaki, huenda ikapoteza points katika ligi ya nyumbani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri : Iddi Ssessanga