AFCON yaanza na ukame wa mabao
17 Januari 2017Jumatatu hii timu hizo zimeshindwa kuonyesha ubabe wao, baada ya Ivory Coast kutoka sare ya bila kufungana na Togo, huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikiibwaga Morocco, bao 1-0.
Ivory Coast inayotetea kombe hilo, iliyotoka sare na Togo, ambayo inashika nafasi ya 21 ya viwango vya soka nyuma ya Ivory Coast, ilicheza kwa kiwango cha kawaida huku mechi hiyo ikikosa msisimko mbele ya mashabiki wachache waliojitokeza kwenye uwanja wa Stade d‘Oyem.
Morocco, ambayo pia inapewa nafasi kubwa ya kushinda michuano hiyo, chini ya kocha Herve Renard, aliyefanikisha kutwaa kombe hilo mwaka 2015 ilipigwa bao 1-0 na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Congo ambayo ilishinda kombe hilo kwa mara ya mwisho miaka 43 iliyopita, Inaongoza kundi C baada ya kujizolea pointi tatu katika raundi ya kwanza.
Ivory Coast na Togo wote zina pointi 1, huku Morocco ambayo ilipata mafaniko makubwa kwenye michuano hiyo mwaka 1976, ikiwa haina pointi yoyote na inaburuta mkia kwenye kundi hilo.
Mechi nne kati ya sita kwenye michuano hiyo zimetoa droo, baada ya Cameroon kukamatwa na Burkina Faso , huku wenyeji Gabon ikitoka sare na Guinea Bissau na Algeria ikitoka sare na Zimbabwe.
Siku ya ufunguzi ilishuhudia, Guinnea Bissau na Burkinafaso zikipanda kwa kasi baada ya matokeo yasiyotarajiwa ya sare ya kutofungana dhidi ya Gabon na Cameroon, katika mechi za kundi A.
Hata hivyo kocha wa Gabon Jose Antonio Camacho alisema ni heshima kubwa kuwa na mchezaji kama Pierre- Emerick Aubameyang katika michuano hiyo katika kujiweka katika nafasi ya kuendelea mbele kwenye michuano kama hiyo.
Aubameyang ameahidi kuiongoza vyema timu yake ambayo ni mwenyeji wa michuano hiyo, baada ya kuanza vibaya, wakati itakapokutana na Burkina Faso Jumatano hii kwenye raundi ya pili ya mechi za kundi A mjini Libreville .
Mechi nyingine za kundi A Jumatano ni Cameroon dhidi ya Guinnea Bissau.
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman