1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD yazipa changamoto siasa za Ujerumani

25 Septemba 2017

Uchaguzi wa Ujerumani umeibua ukweli mchungu kwa wapinzani wa siasa kali za kizalendo kwa wapigakura kukiamini chama kinachofuata siasa hizo, Alternativ für Deutschland (AfD), kuingia kwenye Bundestag,

https://p.dw.com/p/2kg9J
Berlin Nach der Bundestagswahl - AfD
Picha: picture-alliance/dpa/J. Stratenschulte

Alternativ für Deutschland au Mbadala kwa ajili ya Ujerumani (AfD) kinajinasibisha kuwa chama cha cha kizalendo, kidemokrasia na kihafidhina. Hata hivyo, wakosoaji kutoka matapo mengine ya kisiasa wanasema huu ni muungano wa makundi ya wenye siasa kali za mrengo wa kulia. 

Katika kauli kali na ya wazi dhidi ya AfD, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel kutokea chama cha Social Democrats, SPD, alielezea masikitiko yake kuwa "wafuasi wa kweli wa siasa za Kinazi" wataweza tena kurejea katika bunge la taifa, Bundestag.

Akizungumza na waandishi wa habari wa kigeni, mtaalamu mashuhuri wa masuala ya vyama vya siasa nchini Ujerumani, Oskar Niedermayer, alisema kuwa si rahisi kuielezea misimamo ya AfD kwa neno moja. "Mimi nawaita kuwa chama cha wazalendo wa kihafidhina chenye mafungamano makubwa na siasa kali za mrengo wa kulia."

Fasili hii, hapana shaka, inakanganya kidogo. Rahisi yao ni nafasi ya AfD kwenye masuala mbalimbali, yanayoweza kujaa kurasa 76 na huku kikiwa na misimamo mingi kwenye kila kitu, kuanzia masuala ya kodi hadi televisheni ya umma hadi haki za wanyama. 

Ubaguzi dhidi ya wageni ndiyo turufu ya AfD

Lakini utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na taasisi inayoheshimika ya Bertelsmann unaonesha kuwa mada pekee ambayo imekuwa na nafasi ya kukiletea chama hicho wafuasi wengi hapa Ujerumani ni msimamo wake kuhusu wahamiaji.

Infografik Wahlergebnisse AfD POR

Kwenye uchaguzi wa Septemba 24, chama hicho kiliweka kwenye mtandao wake sababu saba kipigia kura - na nne za mwanzo zilikuwa zahusu waomba hifadhi, wahamiaji na Uislamu. Kwa hivyo, jukwaa rasmi la chama hiki linawapa wapigakura kitu kimoja tu - nacho ni hofu na uadui dhidi ya wale wanaochukuliwa kuwa wageni.

"Mchanganyiko wa wakimbizi, ugaidi na usambaaji wa itikadi kali ya Uislamu ndio alama kubwa ya AfD kwa sasa," anasema Niedermayer.

Hilo halimaanishi kwamba wapigakura wote wa AfD ni wale wanaoweza kuwa Manazi, lakini hapawezi kupuuziwa ukweli kwamba chama hiki kinawaona watu wa Ujerumani sio tu kuwa ni wenye thamani kuliko wengine wote, bali zaidi kama kabila maalum lenye utamaduni na mila iliyo bora zaidi, kwa mfano, kuliko watu wa Afrika Kaskazini.

Na hapana mahala ambapo ukweli huu upo wazi zaidi kuliko kwenye kuangalia orodha ya watu ambao AfD imewaweka kuwa wabunge wake watarajiwa.

Matokeo rasmi sasa yashaonesha kuwa AfD ina viti 94 kwenye bunge la shirikisho, Bundestag. Sehemu kubwa ya viti hivyo, kama sio vyote, itapaswa kujazwa na orodha za wagombea kutoka kila jimbo kati ya majimbo 16 ya Ujerumani.

Viongozi wa AfD ni ishara ya chama chao

Deutschland PK AfD
Viongozi wa AfD, Frauke Petry (kulia), Joerg Meuthen (kushoto) na Alice Weidel (wa pili kulia) na Alexander Gauland (wa pili kushoto), alama ya siasa zao.Picha: Reuters/F. Bensch

Wagombea hao wanaaakisi tabia na mitazamo ya chama hicho nchini kote. Vongozi wa chama hicho - Alexander Gauland na Alice Weidel - wamekuwa wakitoa kauli tata na za makusudi kabisa ambazo sasa huenda zikaidhuru nafasi ya chama hicho.

Huko nyuma, wanachama wa AfD, wengi wao wakiwa sasa wana uhakika wa kuwemo kwenye Bundestag, walitangaza  kuwa "katiba haiandikwi kwenye jiwe", wakitaka kukomeshwa kwa kile kiitwacho "ukosaji wa milele" unaozunguka suala la maangamizi ya Mayahudi barani Ulaya, maarufu kama Holocaust, wakionya pia dhidi ya wanachokiita "uundwaji wa watu mchanganyiko" na wakimuita Kansela Angela Merkel na wanasiasa wengine wakubwa kuwa ni "wasaliti kwa watu wao."

Wengi wa wabunge hawa wapya wana mafungamano na makundi madogo madogo ya siasA kali kama NPD na Die Republikaner na pia mavuguvugu ya PEGIDA na Identitarianism - yote yakiwa yanachunguzwa na Ofisi ya Ulinzi wa Katiba.

Hawa ndio watunga sheria wanaokwenda kuingia kwenye bunge lijalo la Ujerumani, na hawa wanatishia misingi ambayo taifa hili inasimamia.

Mwandishi: Jefferson Chase/DW English
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf