1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika CDC tayari kuisaidia Tanzania kudhibiti Marburg

16 Januari 2025

Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimeeleza kuwa kiko tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika na serikali ya Tanzania kuhusu mlipuko wa virusi vya Marburg, iwapo msaada huo utaombwa.

https://p.dw.com/p/4pEuc
Muonekano wa kirusi cha Marburg
Shirika la Afya Duniani(WHO) jan lilitoa taarifa ya kuwepo kwa vifo 9  vilivyotokana na virusi vya Marbug, nchini Tanzania.Picha: Science Photo Library/IMAGO

Hadi sasa, kituo hicho kinasema kinaheshimu msimamo wa serikali ya Tanzania kuhusu suala hilo. Kauli hiyo imetolewa baada ya serikali ya Tanzania kukanusha madai ya kuwepo kwa mgonjwa yeyote aliyepimwa na kuthibitishwa kuwa na virusi vya Marburg katika taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Akizungumza na wanahabari katika mkutano wake wa mwanzo wa mwaka uliofanyika leo, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Africa(Africa CDC) , Dk Jean Kaseya, amesema kituo hicho kinaheshimu maoni ya serikali ya Tanzania kuhusu mlipuko wa virusivya Marbug na hivyo haina la kuongeza.

Kadhalika Dk Kaseya amesema, licha ya kuwa Tanzania inasisitiza kuwa hakuna virusi vya Marbug lakini Africa CDC ipo tayari kutoa msaada wowote ambao Tanzania itauhitaji. Dk Kaseya ameongeza kuwa kabla hata ya kuwepo taarifa hizo za kuwepo kwa virusi vya Marbug, ofisi yake ilishatoa mafunzo kwa wataalamu wa afya  ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Shirika la Afya Duniani(WHO) jan lilitoa taarifa ya kuwepo kwa vifo 9  vilivyotokana na virusi vya Marbug, nchini Tanzania.

Hata hivyo jana usiku, Wizara ya afya kupitia taarifa yake kwa umma ilikanusha kuwepo kwa vifo vilivyosababishwa na virusi hivyo na katika taarifa hiyo Wizara imeeleza kuwa tayari timu ya wataalamu imetumwa mkoani Kagera, kufanya uchunguzi wa kimaabara kubaini iwapo kuna virusi hivyo.

"Mpaka leo tarehe 15 Januari 2025 majibu ya uchunguzi wa kimaabara kwa wahisiwa wote waliochukuliwa sampuli hizo, hayajathibitisha uwepo wa virusi vya Marbug” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri wa Afya Tanzania, Jenista Mhagama.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mwili, Dk Elisha Osati amezungumzia mkanganyiko kati ya WHO na taarifa ya serikali ya wizara ya Afya.

Kwa mujibu wa WHO, wasiwasi wa uwepo wa virusi huo ni mkubwa kwa kuwa mkoa wa Kagera umepakana na nchi za Rwanda na Burundi ambazo kimsingi zimeshakuwa na kesi za virusi hivyo katika kipindi cha mwaka 2023/2024.

Mwaka jana, watu 26 walipoteza maisha nchini Rwanda kutokana na virusi vilivyothibitishwa kimaabara kuwa ni virusi vya Marburg.