1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika inaongoza kwa matumizi ya simu za mkono

Lillian Urio18 Julai 2005

Afrika ndio bara pekee lenye simu za mkono zaidi kuliko simu za kawaida. Mpango wa Ujerumani wa kulisaidia bara hili, kupambana na umaskini, umegundua umuhimu wa simu za mkono.

https://p.dw.com/p/CHfp
Kibanda cha huduma za simu, mjini Dar-Es-Salaam, Tanzania
Kibanda cha huduma za simu, mjini Dar-Es-Salaam, TanzaniaPicha: DW

Simu za mkono kwa baadhi ya watu wa nchi za Magharibi ni sawa na mchezo. Wanachozingatia ni kamera kwenye simu hizo, aina mbalimbali za milio, ambazo sasa hivi wanaweza kuzipata kupitia mtandao na wanatumiana ujumbe au taarifa fupi zisizo na umuhimu.

Watoto wa matajiri katika mabara ya Ulaya na Marekani, wananunua simu za bei ya juu ili kuonyesha uwezo wa familia zao.

Tangu mwaka 1999, shirika la Ujerumani la uwekezaji na maendeleo, DEG, limeweka vitega uchumi katika miradi 6 barani Afrika, ilioyogharimu Euro milioni 80, ya mawasiliano kwa njia ya simu. Baadhi ya nchi zilizonufaika na miradi hiyo ni Nigeria, Tanzania na Uganda.

Moja ya makampuni yaliofaidika ni Celtel, linalo ongoza katika mtandao wa simu za mkono na wateja wake ni asilimia 30 ya wakazi wa Afrika. Kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi nyingi za Afrika zikiwemo Malawi, Burkina Faso, Uganda, Kenya, Sierra Leone na Gabon.

Kwa njia hii bara la Afrika limeweza kukwepa kulazimika kuweka mtandao, wa gharama za juu, kwa ajili ya simu za kawaida. Simu za mkono zina matumizi tofauti kabisa Afrika, ukilinganisha na Ulaya au Marekani. Matthias Goulink kiongozi wa mradi wa DEG anaelezea:

“Lengo letu katika siasa za kuleta maendeleo ni kuwawezesha watu wa Afrika kuwasiliana. Matokeo yake katika jamii ni wanaweza kuinua hali ya maisha yao ya kila siku. Pia kuna manufaa ya kiuchumi, kwa wafanyabiashara wadogo ambao wanaweza kuwasiliana na wateja na kwa upande mwingine wale wanaowapatia bidhaa zao. Pia kuna wafanyabiashara wadogo wanaohusika kwa njia moja wau nyingine na simu za mkono. Kuna wale wanao uza kadi za simu na wengine wana simu za kuwalipisha watu wengine kuzitumia. Kwa njia hizi watu wengi wameweza kujipatia ajira.”

Sio kila mtu mwenye uwezo wa kununua simu za mkono barani Afrika, lakini angalau wanaweza kupiga simu mara chache kila mwezi. Simu za mkono zinahudumia biashara. Bidhaa zinaagizwa, bei za masoko ya karibu zinaulizwa na watu wanaweza kupanga mikutano.

Pia simu hizo zinasaidia wakati wa dharura, kwa mfano kumpigia simu daktari au kuiarifu hospitali kwamba mgonjwa yuko njiani.

Ajira zimepatikana kwa maelfu ya watu kwa biashara za simu za mkono. Kuna wanaokopesha simu hizo, wanaouza kadi za simu na vitu vingine vinavyoendana na simu hizo mfano makasha au mifuko ya simu.

Shirika la DEG, likiwakilisha wizara ya maendeleo ya Ujerumani, linawekeza katika makampuni ya kibinafsi katika nchi zinazoendelea.

Mwaka 2001 shirika hilo liliwekeza katika kampuni ya Celtel na mnamo mwaka 2004 likaongeza hisa zake katika kampuni hiyo, lakini hivi sasa Celtel ina matatizo ya kifedha.

Kwa baadhi ya watu wanaoshiriki katika masuala ya kimaendeleo hawaungi mkono uwekezaji katika makampuni ya kibinafsi. Wanauliza kwa nini wasiwekeze fedha hizo katika makampuni ya Ulaya? Mfano kampuni la mawasiliano kwa nji ya simu la Ulaya.

Bwana Goulink anaamini makampuni ya mawasiliano ya Ulaya yanaogopa yale ya Afrika. Mafanikio ya kiuchumi ya Celtel yamethibitisha kwamba kuna manufaa ya kuwekeza katika miradi kama hiyo. Lakini anasikitika kuna baadhi ya makampuni makubwa yanajitoa katika kuwekeza Afrika na kuelekea Ulaya. Anamatumaini Celtel itakuwa mfano na kuonyesha ukiwekeza Afrika utaweza kufaidika.