1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya20 Julai 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya hali ya kisiasa nchini Misri, wasi wasi wa Rais al-Bashir wa Sudan na juu ya mkasa wa Cecile Kyenge mwafrika wa kwanza kuwa waziri nchini Italia

https://p.dw.com/p/19B3R
Waziri wa masuala ya wahamiaji nchini Italia Cecile Kashetu Kyenge
Waziri wa masuala ya wahamiaji nchini Italia Cecile Kashetu KyengePicha: picture alliance/AP Photo

Gazeti la "Die Welt" limefanya mahojiano na Balozi wa Misri nchini Ujerumani Mohamed Higazy aliesema kuwa jeshi ambalo wiki tatu zilizopita lilimwondoa madarakani Rais Mohammed Mursi, haliwanii kuwa na dhima yoyote ya kisiasa. Gazeti la "Die Welt"limeuliza kwa nini mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi amejipa nyadhifa za Waziri wa ulinzi na Makamu wa Waziri Mkuu?

Balozi Higazy amelijibu swali hilo kwa kuliambia gazeti la "Die Welt" kwamba jeshi la Misri limetamka mara kadhaa kuwa halina haja ya kuwa na dhima katika mambo ya siasa. Balozi huyo ameliambia gazeti la "Die Welt" kuwa kuondolewa madarakani kwa Mohammed Mursi haikuwa hatua ya kuiangusha serikali .Ameeleza kuwa Wamisri zaidi ya Milioni 30 walijitokeza barabarani kutaka masahihisho yafanyike baada ya hatua ya kwanza ya mapinduzi nchini Misri.

Gazeti la "Süddeutsche" pia limechapisha makala juu ya hali ya kisiasa nchini Misri. Katika makala hiyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba uongozi mpya wa kipindi cha mpito,unawakilishwa na watu kutoka pande mbalimbali. Lakini chama cha Udugu wa kiislamu hakiutambui uongozi huo.

Julius Malema arejea katika siasa nchini Afrika Kusini:

Gazeti la "die tageszeitung"limechapisha makala juu ya Julius Malema. Gazeti hilo linafahamisha kwamba Malema amerejea tena katika ulingo wa kisiasa.Kijana huyo aliefukuzwa na chama cha ANC ameunda chama chake.

Malema aliekuwa kiongozi wa tawi la vijana wa ANC anakiita chama chake kuwa ni cha wapigania ukombozi wa kiuchumi-"Economic Freedom Fighters ",EFF. Lengo la chama hicho ni kutawala Afrika Kusini siku moja. Malema amesema chama cha EFF ni cha umma na wao ni serikali inayosubiri kungia madarakani. Chama cha EFF hakijatangazwa rasmi lakini wanachama wake wenye itikadi kali tayari wanataka watu weupe nchini Afrika Kusini wapokonywe hatamu za kiuchumi.

Rais Omar al-Bashiri wa Sudan atimua mbio:

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeandika juu ya Rais wa Sudan Omar Bashir anaetafutwa na mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague,ICC alilazimika kuikatiza ziara yake nchini Nigeria.

Gazeti hilo linaeleza kuwa Rais al-Bashir aliekuwa anahudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika juu ya maradhi ya ukimwi mjini Abuja alizitimua mbio baada ya wanaharakati kutoa mwito kutaka akamatwe. Hata hivyo maafisa walio karibu na Rais huyo wamezikanusha habari hizo. Lakini gazeti ,limeripoti kwamba asasi za kutetea haki za binadamu nchini Nigeria zilitaka Rais huyo akamatwe kutokana na tuhuma za kutenda uhalifu dhidi ya binadamu .Kwa mujibu wa gazeti la "die tageszeitung" Mahakama ya Kimataifa ,ICC pia iliitaka serikali ya Nigeria imkamate kiongozi huyo wa Sudan.

Waziri wa kwanza mweusi nchini Italia afananishwa na sokwe:

Gazeti la "Süddeutsche"limeripoti juu ya mkasa unaomhusu Waziri wa kwanza mweusi katika baraza la mawaziri nchini Italia.

Waziri huyo Cecile Kyenge mwenye asili ya Kongo alifananishwa na sokwe na Seneta mmoja-Roberto Calderoli ambae pia ni naibu wa Spika wa baraza la seneti nchini Italia. Gazeti la "Süddeutsche" limearifu kwamba Waziri Kyenge amesema kauli ya Seneta huyo haikumkashifu yeye,bali imeikashifu Italia.

Gazeti hilo limefahamisha kuwa Seneta Roberto Calderoli ni mwanachama wa chama cha Northern League kinachowakilisha msimamo kwamba mhamiaji aliezaliwa nje ya Italia hawezi kuwa waziri nchini humo. Lakini gazeti hilo pia limaerifu kwamba Seneta huyo ameomba radhi.

Waziri Kyenge mwenyewe amekaririwa akisema kuwa Italia siyo nchi yenye ubaguzi, lakini ameeleza kuwa Italia imechelewa kutambua kwamba ni nchi inayohamiwa sana.Idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa nchini Italia sasa wana nasaba za uhamiaji.

Lakini gazeti la Süddeutsche" limearifu juu ya kauli nyingine mbaya iliyotolewa juu ya mama huyo. Mwanasiasa mmoja wa chama cha Northern League Dolores Valandro ametoa mwito wa kubakwa kwa Waziri Kyenge!

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Yusuf Saumu