1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya15 Novemba 2013

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya kushindakana kwa hatua ya kuutia saini mkataba wa kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

https://p.dw.com/p/1AINP
Waasi wa M23 waliochapwa vizuri
Waasi wa M 23 waliochapwa vizuriPicha: Reuters/Kenny Katombe

Magazeti hayo pia yameandika juu ya mpango wa Kenya wa kuwarudisha kwao wakimbizi wa kisomali na pia yameandika juu ya aliyekuwa katibu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan.

Lakini tunaanza na makala ya gazeti la "die tageszeitung" juu ya kushindikana kutiwa saini kwa mkataba wa kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba hatua ya kuutia saini mkataba huo, ilivurugika katika dakika za mwisho mjini Kampala.

Gazeti la "die tageszeitung" limeukariri ujumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ukisema kwamba mkataba wa amani unapaswa kubadilishwa na badala yake uitwe tamko la amani. Wakati huo huo, gazeti la "die tageszeitung" limetilia maanani kwamba bila ya mkataba wa amani kutiwa saini, kiongozi wa waasi wa M23 Jenerali Sultani Makenga hatapelekwa Kongo ili kuzijibu tuhuma za kutenda uhalifu wa kivita.

Wakimbizi wa kisomali kurudishwa kwao

Gazeti la "Süddeutsche" limeandika juu ya mpango wa serikali ya Kenya wa kuwarudisha kwao wakimbizi wa kisomali nusu Milioni.Gazeti hilo limetilia maanani kwamba mpango huo unafuatia mkasa uliotokea kwenye jengo la biashara la Westgate mjini Nairobi hivi karibuni. Magaidi wa al-shabaab waliwateka nyara na kuwaua watu kadhaa. Gazeti la "Süddeutsche" linaeleza katika makala yake kwamba hasira za wakenya zinaelekezwa kwa wahamiaji. kila yanapotokea mashambulio nchini mwao. Wahamiaji wamekuwa wanatuhumiwa. Hali imekuwa hivyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Gazeti la "Süddeutsche " limemnukulu mwenyekiti wa kamati ya bunge la Kenya inayoshughulikia usalama wa taifa, Asmam Kamama, akisema kuwa kambi ya wakimbizi ya Dadaab imegeuka kuwa mbegu ya kuzalishia ugaidi.

Kenya imetilialiana saini na serikali ya Somalia na Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, mkataba juu ya kuwarudisha nyumbani wakimbizi hao laki tano. Mpango huo umepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kofi Annan apewa tuzo ya Bartelsmann

Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ametunukiwa tuzo ya Reinhard Mohn ya Wakfu wa Ujerumani wa Bartelsmann kwa mchango wake katika harakati za kutetea maendeleo ya kudumu na haki za binadamu. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Süddeutsche" mnamo wiki hii. Bwana Annan anaetokea Ghana alikabidhiwa tuzo hiyo katika mji wa Gütersloh nchini Ujerumani. Katika mahojiano na gazeti hilo Kofi Annan alizungumzia juu ya kushindwa kwa serikali katika suala la ulinzi wa mazingira.

Na kwa ajili hiyo ametoa mwito kwa wananchi wenyewe wasimame katika mstari wa mbele ili kuongoza juhudi za kuleta maendeleo.

Jee almasi za Afrika zinaleta nini kwa Waafrika?

Jee ulijua kwamba biashara ya almasi inaingiza jumla ya dola Bilioni 72 kila mwaka duniani?. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii. Gazeti hilo limeikariri taarifa ya Baraza la dunia linaloyasimamia maslahi ya wafanya biashara wa almasi. Kwa mujibu wa Baraza hilo, kila mwaka almasi thamani ya dola Bilioni 13 zinazalishwa, na asilimia 65 ya almasi hizo zinatoka barani Afrika.

Gazeti hilo pia limeandika juu ya almasi maarufu iliyouzwa kwenye mnada mjini Geneva kwa thamani ya dola 83 na laki mbili. Almasi hiyo iliyouzwa jumatano iliyopita inatoka katika mgodi mmoja wa Afrika kusini.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Josephat Charo