Afrika katika magazeti ya Ujerumani
22 Septemba 2017Gazeti hilola Süddeutsche Zeitung limeandika kwamba ilikuwa kama hadhithi ya alfu lela ulela. Katika picha za arusi mtu anaweza kuwaona wanaume waliovaa kofia za tarabushi na wanawake waliovaa magauni marefu yaliyometameta.Watu hao wanaonekana wamesimama mbele ya hoteli ya kifahari katika mji wa Sun City. Miaka 20 tu iliyopita ndugu watatu wa familia ya Gupta walihamia Afrika Kusini kutoka India wakiwa makapuku-mifuko mitupu. Lakini leo ndugu hao watatu ni matajiri wakubwa nchini Afrika Kusini wanamiliki viwanda vya chuma na nishati. Gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung linaeleza kwamba utajiri wa akina Gupta unatokana na umahiri wao wa kuwapata marafiki sahihi na hasa Rais Jacob Zuma. Mtoto wa Zuma alifanya mafunzo kwenye kampuni mojawapo ya akina Gupta. Kutokana na urafiki huo kampuni za akina Gupta zilikuwa za mwanzo kabisa kujihakikishia hisa. Wigo wa kashfa ya ufisadi umetanuka hadi nchini Ujerumani Gazeti hilo linasema Kampuni ya Ujerumani ya programu za kompyuta SAP inadaiwa kuwa iliwalipa fedha akina Gupta.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limeandika taarifa juu ya mchango wa Ujerumani katika kupambana na ugaidi kwenye ukanda wa Sahel. Frankfurter Allgemeine linaeleza kuwa Ujerumani kwa kushirikiana na Ufaransa zinaunda kikosi cha kupambana na ugaidi kwenye eneo la Sahel. Askari hao wanatoka Mauritania, Mali, Niger, Burkina Faso na Chad. Kikosi hicho cha askari 5000 kinaweza kupelekwa katika nchi yoyote ya ukanda wa Sahel ili kwenda kuwakabili magaidi. Mpango wa kuunda jeshi hilo ulipitishwa na nchi hizo mnamo mwezi wa Julai. Wajumbe kutoka nchi hizo za Sahel walishiriki kwenye mkutano wa matayarisho uliofanyika mjini Berlin hivi karibuni. Ujerumani itashiriki kwa kutoa mafunzo kwa askari hao watakaopambana na magaidi. Wakati Ujerumani itashiriki katika mradi huo kwa kutoa mafunzo, Umoja wa Ulaya unatafakari kutoa msaada wa fedha wa hadi Euro milioni 50 kwa ajili ya nchi hizo tano za ukanda wa Sahel.
Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger limeandika juu ya mwandishi wa riwaya wa Zimbabwe Petina Gappah. limemnukuu akisema nchi yake imetengwa na dunia nzima. Mwandishi huyo ambaye sasa anaishi katika jiji la Berlin anayazingatia masuala ya ukoloni na ubagauzi wa rangi katika vitabu vyake. Mwandishi huyo ametumia lugha ya mafumbo kuandika juu ya mtu aliyetengwa akimaanisha hali ya kisiasa inayoikabili nchi yake Zimbabwe ambayoanasema kwa sasa imetengwa na nchi nyingi duniani. Mwandishi riwaya Petina Gappah kutoka Zimbabwe ameeliambia gazeti hilo la Kölner Stadt-Anzeiger kwamba raia wa Zimbabwe ni sawa na watu waliofungiwa ndani na kutengwa na dunia. Hata hivyo mwandishi wa riwaya huyo ameeleza kwamba ana matumaini nchi yake itabadilika kwa sababu Rais Mugabe hataendelea kutawala kwa muda mrefu zaidi kutokana na umri wake wa miaka 93.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung limeandika juu ya juhudi za wanasheria wa Afrika za kuiondoa kasumba iliyobakia kwenye vichwa vya wahusika kwenye sekta ya sheria, gazeti hilo linasema kuanzia Kenya, Zimbabwe hadi Nigeria mahakimu bado wanavaa mawigi wanapokuwa mahakamani. Mabaki ya kasumba hiyo ni kutokea enzi za ukoloni wa Waingereza. Mahakimu, wanaharakati na wanasiasa wanaendesha kampeni yenye lengo la kuutupilia mbali utamaduni huo wa kuvaa mawigi.
Mwandishi: Zainab Aziz/ Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman