Afrika katika magazeti ya Ujerumani
13 Oktoba 2017Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba jumuiya ya kimataifa inawataka wanasiasa nchini Kenya wawe na busara. Gazeti hilo linasema utulivu uliopo baada ya matokeo ya uchaguzi kubatilishwa hauwezi kudumu kwa muda mrefu. Gazeti hilo linaeleza kuwa kila siku za jumatatu na ijumaa wafuasi wanaomuunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga wanafanya maandamano nchini Kenya ya kutaka kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi lakini polisi nao wanafanya kazi yao. Ijumaa iliyopita polisi hao walitumia gesi ya kutoa machozi mjini Nairobi ili kuwakabili waandamanaji. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema hali nchini Kenya ni ya kutia wasiwasi na ndiyo sababu mabalozi wa nchi kadhaa miongoni mwao balozi wa Ujerumani wamewataka viongozi wa Kenya waishughulikie hali ya sasa kwa busara.
Magazeti yanasemaje juu ya Zimbabwe?
Nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe amefanya mabadiliko ya baraza la mawaziri. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwa nini Mugabe amechukua hatua hiyo. Zimbabwe inaendelea kuzama katika lindi la matatizo ya kiuchumi lakini badala ya kuchukua hatua ili kuondokana na hali hiyo rais Robert Mugabe anaelekeza juhudi zake katika kumuandalia mkewe urithi wa wadhifa wa urais. Katika mabadiliko aliyoyafanya Mugabe amemuondoa Makamu wake, Emmerson Mnangagwa kwenye wadhifa wa waziri wa sheria. Mnangagwa anazingatiwa kuwa hasimu mkubwa wa mke wa rais Mugabe, bi Grace. Lengo la Mugabe ni kuwafyeka mahasimu wa mkewe. Watu nchini Zimbabwe wananong'ona kwamba Grace Mugabe atatangazwa kuwa mrithi wa kiti cha mumewe kwenye mkutano mkuu ujao wa chama tawala cha Zimbabwe Zanu PF. Juu ya mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Mugabe, gazeti limemkariri katibu mkuu wa chama cha kikomunisti cha Zimbabwe Ngqabutho Mabhena, anaeishi katika hifadhi huko nchini Afrika Kusini, akisema mabadiliko hayo hayatayatatua matatizo ya Zimbabwe.
Yaliyojiri nchini Liberia wiki iliyopita
Gazeti la die tageszeitung wiki hii pia limendika juu ya rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia. Linasema baada ya kuiongoza Liberia kwa muda wa miaka12 mama huyo ameng‘atuka. Hata hviyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba Ellen Johnson Sirlef alikuwa anaheshimiwa sana kimataifa, lakini utendaji kazi wake ndani ya Liberia ulikuwa unakosolewa sana. Lakini vilevile gazeti hilo linamsifu Ellen Johnson Sirleaf kwa kuheshimu katiba. Linasema mama huyo hakuwa na mawazo ya kuibadilisha katiba ili kuendelea kung'ang'ania madarakani, jambo ambalo limekuwa la kawaida miongoni mwa viongozi kadhaa barani Afrika. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba Ellen Johnson Sirleaf hakuweza kuitimiza ahadi ya kuung'oa ufisadi katika miaka 12 ya uongozi wake.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman