Afrika katika magazeti ya Ujerumani
24 Januari 2020Die Welt
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya nje Heiko Maas wameboronga juu ya Libya. Ni kweli kwamba diplomasia ya makini ni muhimu na ndiyo sababu Ujerumani imechangia kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika mjini Berlin. Hata hivyo makosa ya kimkakati yamefanyika. Kwa kutumia lugha ya kandanda tunaweza kusema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya nje Heiko Maas wamejifunga goli wenyewe.
Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba watakaonufaika na matokeo ya mkutano huo ni Rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Uturuki Tayyip Erdogan. Gazeti hilo linasema inaafaa kukumbuka kwamba Urusi na Uturuki zinaunga mkono pande mbili tofauti zinazohusika na magogoro wa nchini Libya. Kwa hivyo katika diplomasia ya nipe nikupe, maslahi ya Putin na ya Erdogan yamezingatiwa.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine limendika juu ya Isabel dos Santos binti yake aliyekuwa rais wa Angola, Dos Santos. Gazeti hilo linazisuta nchi za Ulaya kwa kueleza kwamba uovu wa ufisadi unahitaji pande mbili, mtoaji na mpokeaji. Kwa muda wa miaka mingi Isabel dos Santos alikuwa anakaribishwa kwa taadhima kwenye mikutano ya kimataifa na kwa muda wa miaka mingi makampuni ya nchi za magharibi yalikuwa yananufaika kwa kufanya biashara na mama huyo mwenye umri wa miaka 46. Kwa muda mrefu makampuni hayo ya magharibi hayakutaka kujua utajiri wa mama huyo ulitokea wapi. Ndiyo sababu, kufichuliwa kwa habari juu ya ufisadi wake kunazikumbusha nchi za Ulaya kile ambacho zinasahau inapohusu Afrika, kwamba ufisadi unahitaji pande mbili, za mtoaji na mpokeaji.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung wiki hii limechapisha makala juu ya juhudi zinazofanywa na jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kupambana na kundi la waasi wa ADF mashariki mwa nchi hiyo. Gazeti hilo linasema jeshi la Kongo linazidi kupata mafanikio katika mapambano hayo. Tangu mwaka 2014 waasi wa ADF wamekuwa wanafanya mauaji ya raia mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Kulingana na makadirio watu wapatao 1600, raia na wanajeshi kadhalika, wameshauawa hadi sasa kutokana na mashambulio yanayofanywa na waasi hao wa ADF. Na kati ya watu hao 150 waliuawa mnamo miezi ya Novemba na Desemba.
Gazeti hilo la die tageszeitung linatueleza kwamba kundi hilo la waasi lilianzishwa nchini Uganda mnamo mwaka 1966 na kuhamia katika nchi jirani ya Kongo. Kutokana na kundi hilo kuongozwa na mtu mwenye itikadi kali, Musa Baluku serikali ya Kongo inatuhumu waasi hao wana mahusiano na kundi linalojiita dola la kiislamu IS. Gazeti la die tageszeitung linaeleza zaidi kwamba kutokana na tuhuma juu ya waasi wa ADF kuwa na uhusiano na kundi linalojiita dola la kiislamu, serikali ya Kongo imeomba msaada kutoka Urusi, Ubelgiji, Ufaransa na Marekani. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linasema, wataalamu wa Umoja wa Mataifa walipofanya mahojiano na mateka wa ADF, hawakuweza kuthibitisha iwapo kundi hilo lia uhusiano na kundi linalojiita dola la kiislamu.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia janga la nzige waliovamia sehemu kadhaa mashariki mwa Afrika. Gazeti hilo linasema wadudu hao wanahatarisha ugavi wa chakula. Mamilioni ya nzige yanavamia mashamba katika eneo lipatalo kilometa 150 kwa siku. Nzige hao wameshavamia maeneo ambayo wanaishi watu zaidi ya milioni 170 katika nchi za Ethiopia, Somalia na Kenya. Uvamizi wa nzige hao ni tishio kubwa kwa uhai wa mamilioni ya watu. Hatua za haraka zinahitajika limesema shirika la chakula la Umoja wa Mataifa FAO kwani wadudu hao wamo njiani kuelekea kwenye sehemu nyingine za Afrika Mashariki.
Vyanzo:Deutsche Zeitungen