1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu Mhariri: Rashid Chilumba
10 Mei 2024

Miongoni mwa masuala ya Afrika yaliyopewa umuhimu na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni habari kuhusu vifo vya watu 35 baada ya mashambulizi katika kambi ya wakimbizi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4fiEm
Magazeti ya Ujerumani
Magazeti ya UjerumaniPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

die tageszeitung

Gazeti hili wiki hii liliimulika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Huko, uko, kunaripotiwa kuwa wakimbizi 35 waliuwawa baada ya kambi yao kushambuliwa. Miongoni mwao ni watoto sita. Watu wengine 37, walijeruhiwa. Gazeti hilo linaeleza kuwa kutokana na shambulio hilo, Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wanatuhumiana kuhusika na shambulio hilo lililotokea nje kidogo ya mji wa Goma.

die tageszeitung lilifafanua kuwa, zaidi ya watu 200,000 wanaishi katika kambi hiyo ya wakimbizi yenye msongamano mkubwa.Watu hao ni wale walilolazimika kuyahama makazi yao na kuweka kambi katika eneo hilo baada yakuizunguka milima katika mji wa Goma ili kupata mahali salama.

Wakimbizi hao walikimbia baada ya kuibuka kwa mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lakini sasa, nao wanalengwa katika vita hivyo. Katika miezi ya hivi karibuni, waasi hao wamefanikiwa kudhibiti eneo kubwa la mkoa wa Kivu kaskazini.

Neue Zürcher na Zeit Online

Magazeti kadhaa ya Ujerumani yakiwemo Neue Zürcher na Zeit Online yaliandika kuhusu uchaguz wa Chad ambao matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa hilo ya uchaguzi mwishoni mwa juma ilimtangaza mshindi  Mahmat Deby.

Kuhusu uchaguzi huo, Gazeti la Zeit Online mwanzoni mwa juma liliandika kuwa, uchaguzi wa rais ambao umekuwa ukiakhirishwa mara kwa mara, sasa umefanyika Chad. Jenerali Mahmat Deby aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka mitatu anataka kuwa Rais. Lilieleza kuwa Derby Anayo nafasi nzuri. Moja ya sababu ni kuwa, mpinzani wake mkubwa, aliuwawa mwezi Februari.

Gazeti hilo lilikwenda mbali zaidi na kusema kwamba, uchaguzi huo wa Chad, ulitazamiwa kumaliza utawala wa wa kijeshi wa miaka mitatu chini ya Rais wa mpito, Mahamat Déby. Taifa hilo lililokuwa koloni la Ufaransa na lenye wakaazi wasiopungua milioni 19, halijawahi kuwa na makabidhiano ya madaraka yenye amani.

Mahamat Deby Itno
Mahamat Deby Itno ameshinda katika uchaguzi wa Urais ChadPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Itakumbukwa kuwa Rais wa sasa Mahmat Deby, aliingia madarakani baada ya baba yake aliyetawala kwa zaidi ya miongo mitatu kuuwawa na waasi.

die tageszeitung

die tages zeitung liliandika juu ya  hatua ya vikosi vya usalama vya Tunisia kuzivamia kambi mbili na kuwafurusha wakimbizi kwanguvu katika mji mkuu Tunis. linaeleza kuwa, wakazi kadhaa wa kambi hizo walifanikiwa kuwatoroka polisi na kukimbilia katika maeneo mengine ya mji.

Taarifa zaidi zinadai kuwa mamia ya watu waliwekwa katika mabasi na kupelekwa katika mji wa Jendouba mpakani na Algeria na kutelekezwa huko. Baadhi ya waathiriwa wa tukio hilo wamesema kuwa miongoni mwa waliotelekezwa mpakani ni pamoja  na wanawake na watoto.

Kambini, matingatinga yalibomoa kambi hizo zisizo rasmi za wakimbizi ambazo zimekuwepo kwa miaka kadhaa. Gazeti hili liliripoti kuwa,  Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa mataifa la UNHCR na Shirika la Kimataifa Uhamiaji la IOM wala hayakujitokeza kupinga hatua hiyo ya wakimbizi kufukuzwa.

die tageszeitung linafichua kuwa, wanadiplomasia wa kimataifa na vyama vya kiraia nchini Tunisia, hawaruhusiwi kuwatembelea wakimbizi wanaoishi katika mazingira magumu na machafu yasiyomithilika. Yeyote anayekutwa karibu na kambi za wakimbizi akiwa na dawa au msaada hufukuzwa na kutishiwa kufunguliwa kesi ya jinai. Tangu mwaka uliopita, Raia wa Tunisia walipigwa marufuku kuwapa vibarua  kupangisha nyumba zao kwa  wahamiaji.

Süeddeutsche zeitung

Süeddeutsche zeitung  liliimulika hali ya kisiasa Afrika ya kusini na masaibu yanayokikabili chama kipya cha upinzani nchini humo. Chama hicho cha uMkhonto weSizwe (MK) cha rais wa zamani Jacob Zuma, ambacho ni tishio zaidi kwa chama tawala  cha ANC kinahusishwa na tuhuma nzito za kughushi sahihi.

Afisa wa juu wa aliyefukuzwa ndani ya chama hicho Lennox Ntsondo ametoa ushahidi kuwa, takribani saini 15,000 zilizohitajika ili kukiruhusu chama hicho kishiiriki uchaguzi zilighushiwa.  Kulingana na shutuma hizo zinazomhusisha pia Nsondo mwenyewe, wanaharakati wa chama hicho cha Zuma waliiba taarifa za watu wanaotafuta kazi kutoka katika kanzidata rasmi bila ya wahusika kufahamu. 

Kisha, majina hayo na anuani vilitumika kwa ajili ya kupata orodha ya sahihi ambazo mwisho wa siku zilikabidhiwa kwa tume ya uchaguzi.  Mkuu wa polisi Afrika ya Kusini Fannie Masemola amethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea mjini Capetown kunakodaiwa kuwa udanganyifu huo wa saini ulifanyika.

Chama kipya cha Zuma kinakabiliwa na tuhuma za udanganyifu
Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini, Jacob ZumaPicha: Michele Spatarii/AP Photo/picture alliance

Wataalamu wanasema kughushi saini ni sawa na wizi wa utambulisho. Kosa la aina hii nchini Afrika ya Kusini linaweza kugharimu faini ya Randi milioni kumi sawa na euro laki tano na kifungo cha hadi miaka 10 jela. Ikiwa sheria itakitia hatiani chama cha MK kwa makosa hayo, basi kitaondolewa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi.

Zeit online

Moja ya habari katika gazeti la Zeit online, wiki hii ilihusu hatua ya makanisa ya Ujerumani kukikosoa chama cha kihafidhina cha CDU kwa kutaka kuweka kipengele cha udhibiti wa wahamiaji kutoka nchi  za dunia ya tatu  hasa Afrika katika ilani yake.

Wazo hilo linafanana na mpango wa hivi karibuni wa Uingereza wa kuwapeleka Rwanda wahamiaji walioingia nchini humo kinyume cha sheria. Gazeti hilo linaarifu kuwa, wawakilishi wa makanisa ya Ujerumani wanakituhumu chama hicho kwa kukiuka maadili ya Kikristo wanaosema kuwa, mtu yeyote anayeongozwa na mtazamo wa Kikristo kuhusu utu, hapaswi kuondoa uwezekano wa wakimbizi kupata ulinzi ndani ya Ulaya.

Makamishna wa wakimbizi wa Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiprotestanti yanakituhumu chama hicho cha CDU kwa kukiuka misingi yake ya kuwalinda wakimbizi. Chama hicho kinataka yeyote anayeomba hifadhi Ulaya apelekwe katika nchi inayodhaniwa kuwa ni salama katika mataifa masikini.