Afrika katika picha: Matukio makuu ya 2017
Marais wa muda mrefu wa Zimbabwe na Gambia waliondolewa mamlakani; ghasia za baada ya uchaguzi Kenya na Liberia; mashambulizi ya kigaidi Somalia na Nigeria. DW inaangazia matukio muhimu yaliyogonga vichwa vya habari 2017
Dikteta wa Gambia Jammeh alipoteza udhibiti wa mamlaka
Yahya Jammeh alikuwa ameiongoza nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi kwa mikono ya chuma kwa miaka 22 hadi alipopoteza uchaguzi wa rais bila kutarajia mwaka 2016 kwa mshindani wake Adama Barrow. Vikosi vya ECOWAS vilitumwa Gambia kumshawishi Jammeh kukubali kushindwa na ajiuzulu. Januari 2017 aliondoka na kwenda uhamishoni Guinea ya Ikweta, lakini baada ya kuivuruga hali ya fedha ya nchi hiyo.
Uganda ilisimamisha msako dhidi ya kiongozi wa waasi Kony
Joseph Kony, ambaye ni mkuu wa kundi katili la waasi la "Lord's Resistance Army" (LRA), anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu. Mnamo Aprili, Uganda na Marekani zilitangaza zitasitisha operesheni ya kumsaka Kony kwani kundi lake la LRA halina nguvu na limekosa maana. Lakini Umoja wa Mataifa umehusisha visa vipya vya utekaji nyara DRC na kundi hilo.
Hofu ya kuitumbukiza Nigeria katika machafuko
Nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, iliathiriwa kwa miezi mitatu kufuatia hali ya kutokuwepo kwa rais Muhamadu Buhari mwenye umri wa miaka 74, wakati ambapo alikuwa London kwa matibabu. Kundi la wanamgambo wa Kiislamu Boko Haram lilifanya mashambulizi ya mara kwa mara Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, eneo ambalo mamilioni ya watu wanategemea chakula cha misaada.
Mzozo wa Cameroon uliongezeka
Watu kadhaa waliuawa na wengi walijeruhiwa kufuatia tangazo la Oktoba, ambalo liliashiria uhuru wa eneo la Wacameroon wanaotumia Kiingereza. Waangalizi wa kimataifa walisema watu 40 waliuawa kwenye makabiliano. Eneo lililoko Kusini Magharibi mwa nchi hiyo lilitangaza uhuru wa jimbo lao la "Ambazonia" kwa sababu watu katika eneo hilo walihisi kutengwa na raia walio wengi wanaozungumza Kifaransa.
Ghasia baada ya chaguzi zenye ushindani mkali Kenya
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliapishwa kwa muhula wa pili, lakini kiongozi wa upinzani Raila Odinga alikataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi. Awali, Mahakama ya Juu nchini humo iliubatilisha uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti kufuatia kasoro zilizojitokeza. Baadaye upinzani ulisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba. Kulitokea ghasia na watu kadhaa waliuawa.
George Weah ashinda uchaguzi wa rais Liberia
Mwanasoka wa zamani wa kimataifa nchini Liberia George Weah alishinda uchaguzi wa marudio kumpata mrithi wa rais wa Ellen Johnson Sirleaf. Weah alimshinda mshindani wake Joseph Boakai ambaye alikuwa makamu wa rais. Uchaguzi wa marudio uliahirishwa baada ya vyama 2 kuwasilisha malalamishi kwa tume ya uchaguzi kuhusu madai ya rushwa katika uchaguzi wa Oktoba. Lakini madai hayo yalitupiliwa mbali.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan Kusini vyazidisha njaa
Katika miaka 4 iliyopita, watu katika taifa changa kabisa duniani- Sudan Kusini wameteseka kufuatia vita kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar. Theluthi ya raia wamelazimika kuyakimbia makwao. Takriban watu milioni tano, (nusu ya idadi jumla ya nchi hiyo) wanakumbwa na njaa. Umoja wa Mataifa umesema mashamba yanayoweza kukuza kilimo yameharibiwa kufuatia vita.
Somalia ilipata shambulio baya zaidi katika historia yake
Lori lililojaa vilipuzi lililipuka katika njia panda yenye shughuli nyingi mjini Mogadishu, katikati ya mwezi Oktoba na kuwaua mamia ya watu. Hadi sasa hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo ambalo limeelezwa kuwa baya zaidi katika historia ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Serikali inalilaumu kundi la al-Shabaab kwa shambulio hilo.
Hakuna Amani kwa Mali
Taifa hilo la Afrika Magharibi limezongwa na mizozo kwa miaka sita: Kwanza ni mapinduzi, kisha kuibuka kwa wanaotaka kujitenga kutoka Kaskazini, ikafuatwa na wanamgambo wa Jihadi. Wanajeshi 11,000 wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa wameshambuliwa mara kadhaa. Januari, wanajeshi 77 waliuawa katika shambulio baya zaidi. Wapiganaji wenye mafungamano na Al-Qaeda walidai kuhusika.
Mtawala wa kidikteta Mugabe aondolewa madarakani
Baada ya utawala wake wa miaka 37, jeshi la Zimbabwe lilimweka Rais Robert Mugabe katika kizuizi cha nyumbani, alipomfuta kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa ili kumweka mke wake katika nafasi ya kuwa mrithi wake. Mugabe alijiuzulu wakati mchakato wa kumuondoa madarakani ulikuwa ukiendelea. Mnangagwa aliapishwa kama rais, lakini amewafelisha wengi waliotarajia angewajumuisha wapinzani serikalini.
Kabila ang’ang’ania mamlaka
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari amehudumu mihula yake miwili inayokubalika kulingana na katiba ya nchi hiyo. Japo muhula wake wa pili ulimalizika mwisho wa 2016 ameendelea kuuahirisha uchaguzi mpya. Uchaguzi sasa umeratibiwa kufanyika mwisho wa 2018. Makundi ya upinzani yamesema polisi wamekandamiza maandamano na kuwakamata waandamanaji.
Rushwa yapanuka Afrika Kusini
Madai ya rushwa yanayomhusu rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na familia tajiri ya Gupta ilishika kasi mwaka 2017. Kampuni za kimataifa zililaumiwa kwa kutoa hongo ili kupata zabuni au kandarasi za serikali. Uchumi wa nchi unaathirika huku viwango vya ukosefu wa ajira vikiwa takriban asilimia 30. Ushindani wa nani kumrithi Jacob Zuma unatarajiwa kushika kasi 2018.