Marekani yakosoa kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel
4 Januari 2024Mahakama hiyo ya ICJ yenye makao yake mjini The Hague inatarajiwa kuanza kusikiliza kesi hiyo wiki ijayo baada ya Afrika Kusini kudai kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.
Soma pia: Israel yaongeza mashambulizi ya anga na ardhini Gaza
Lakini msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House, John Kirby ameiita kesi hiyo kuwa "isiyo na maana, wala tija na haina msingi wowote kwa ukweli."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Matthew Miller kwa upande wake ameelezea wasiwasi juu ya madai hayo na kusema kuwa hadi sasa hawajashuhudia chochote kinachoashiria mauaji ya kimbari.
"Mauaji ya kimbari hakika ni uhalifu wa kutisha," Miller aliwaambia waandishi wa habari. "Haya ni madai ambayo hayatakiwi kutolewa kirahisi rahisi tu."
Afrika Kusini, ambayo mara kwa mara imeikosoa Israel kwa namna inayvowachukulia Wapalestina, imeyafananisha matukio yanayofanywa na Israel na historia ya utawala wa kibaguzi nchini humo, na kuishutumu kwa kufanya visa hivyo kwa malengo maalumu ya "kuwaangamiza Wapalestina walioko huko Gaza ambao ni sehemu ya kundi kubwa la taifa, rangi na jamii ya Palestina."
Afrika Kusini inataka kutolewa amri itakayoilazimisha Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Katika hatua nyingine, Ujerumani na Ufaransa zimekosoa matamshi yaliyotolewa na mawaziri wawili wa serikali ya siasa kali za mrengo wa kulia nchini Israel waliopendekeza kwamba vita vya Gaza vinaweza kusababisha watu wa Palestina kuishi kwenye makaazi mapya.
"Tunapinga vikali kauli zilizotolewa na mawaziri hao wawili. Hazina busara wala hazisaidii," Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilisema maoni ya Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir "hayaonyeshi uwajibikaji na yanachochea mivutano."