Afrika Kusini yatoa wito wa amani nchini Zimbabwe
29 Agosti 2023Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema nchi yake imezingatia ripoti ya waangalizi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC juu ya uchaguzi uliokamilika wa Zimbabwe, na kuzitaka pande zote nchini humo kushirikiana.
Ujumbe wa SADC ulielezea wasiwasi wao juu ya ucheleweshwaji wa zoezi la kupiga kura, kupigwa marufuku kwa mikutano ya hadhara ya upinzani, pamoja na upendeleo wa vyombo vya habari katika kuripoti huku waangalizi wa Umoja wa Ulaya wakisema kuwa, uchaguzi wa Zimbabwe ulifanyika katika "mazingira ya hofu."
Kauli ya Ramaphosa imeonyesha kuwa serikali yake iko tayari kusaidia kutatua mvutano wowote utakaojitokeza kati ya serikali ya Zimbabwe na upinzani.
Tume ya uchaguzi ilimtangaza Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80 kama mshindi japo wachambuzi wametilia shaka uhalali wa matokeo hayo.