Afrika Kusini: Rais anaepambana na watu wake
6 Mei 2022Ni wafanyakazi wachache waliojitokeza kumsikiliza Rais Cyril Ramaphosa katika mkutano wa Mei Mosi katika Jimbo la Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini mapema wiki hii. Wale waliohudhuria walimshambulia kwa nyimbo zilizotaja "Cyril lazima aondoke!"
Makabiliano hayo na rais katika Uwanja wa Royal Bafokeng siku ya Jumapili yalihusisha wafanyakazi wengi waliofanya mgomo katika mgodi wa dhahabu wa Sibanye-Stillwater ulio karibu na Rustenburg pamoja na wale wanaounga mkono madai ya wachimba migodi hao ya kutaka malipo bora zaidi.
Soma pia: Chama cha ANC chagawika kuhusu uchunguzi wa rushwa
Kitendo cha Ramaphosa kurudi haraka katika lori la polisi lililokuwa na silaha kilionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni.
Herman Mashaba, meya wa zamani wa jiji la Johannesburg na kiongozi wa chama cha ActionSA, ameuambia mtandao wa habari wa News24 kuwa hakuamini wakati jambo hilo lilikuwa likiendelea.
Siku chache baada ya Ramaphosa kuzomewa jukwaani, chama tawala cha African National Congress (ANC) na washirika wake wa jadi na hata wafuasi wake wamekuwa wakishughulika kudhibiti hali hiyo.
Kwa haraka, Ramaphosa alitoa taarifa akielezea haja ya kuwepo suluhu la haki la mishahara kwa wachimbaji hao. Ramaphosa aliandika katika jarida wiki hii kuwa, malalamiko ya mishahara ya wafanyakazi huko Rustenburg yanastahili kuzingatiwa na wadau wote, waajiri na wafanyakazi ili suluhu ya haki na endelevu iweze kufikiwa huku akiongeza kuwa, kama serikali, wamejitolea kutekeleza jukumu lao.
Wakati muafaka
Lakini wengi walikataa kuamini ahadi hizo na kusema wanaunga mkono hatua za umati za kumpinga Ramaphosa katika hafla za Mei Mosi.
Vyama vya siasa na wachambuzi wanafuatilia kwa makini hali hiyo. Sio tu kwamba uchaguzi mdogo wa manispaa unaendelea kwa sasa katika majimbo matatu, lakini vita vya ndani vya mamlaka vinapamba moto ndani ya ANC, na Ramaphosa anakabiliwa na jitihada za kuchaguliwa tena kama kiongozi wa chama hicho mwaka ujao.
Soma pia: Maoni: Machafuko Afrika Kusini yafichua kushindwa kwa serikali
Brian Sokotu, ripota wa kisiasa mwenye makazi yake huko Johannesburg anaeleza kuwa, hatua kwa hatua Ramaphosa anapoteza uaminifu miongoni mwa wafanyakazi ambao wanataka masuala nyeti yashughulikiwe na serikali.
Vyama viwili vikubwa vya migodi vinadai nyongeza ya mishahara ya randi 1,000 ikiwa ni sawa na dola 63 kwa mwezi katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, huku uongozi wa mgodi huo ukitaka kuwapa wafanyakazi wake nyongeza ya randi 800 pekee.
Jeraha lililo wazi
Wafanyakazi waliokuwa na hasira katika Mkoa wa Kaskazini Magharibi huendesha shughuli zao katika eneo lililo karibu na mgodi wa Marikana ambako mwaka 2012, polisi waliwaua kwa risasi wachimba migodi 34 waliokuwa kwenye mgomo na kuwajeruhi vibaya wengine kadhaa.
Soma pia: Ramaphosa asema vurugu zilichochewa na watu fulani
Wakati huo, Ramaphosa alikuwa mkurugenzi asiye mtendaji wa Lonmin, shirika la kimataifa lililokuwa likiongoza Marikana. Lonmin, ambayo tangu wakati huo imenunuliwa na Sibanye-Stillwater, ilipendelea kutumia mabavu katika uingiliaji kati ili kumaliza mgomo huo.
Mauaji hayo yaliashiria tukio baya zaidi Afrika Kusini baada ya ubaguzi wa rangi na raia wengi bado hawajakubali kauli za msamaha zilizotolewa hapo awali na rais Ramaphosa.
Wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi, Ramaphosa alikuwa kiongozi wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi wa Migodini (NUM). Alijulikana mno kwa kupenda maisha ya kifahari, kufurahia mvinyo na tabia yake ya kupanda ndege daraja la kwanza.
Alijikusanyia mali nyingi chini ya mipango ya kuwawezesha Weusi kiuchumi baada ya kumalizika kwa utawala wa watu weupe walio wachache mnamo mwaka1994. Leo utajiri wa Ramaphosa unakadiriwa kuwa dola za Marekani milioni tatu.
Miaka minne katika ukurasa mpya
Baada ya Ramaphosa kushinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2018, Waafrika Kusini walikuwa na matumaini kwamba kutokana na uzoefu wake mkubwa katika ulimwengu wa wafanyabiashara wakubwa, angeweza kukuza haraka na vya kutosha uchumi wa nchi hiyo na kuwaondoa watu wengi katika umaskini.
Soma pia: Vurugu zaendelea Afrika Kusini baada ya kufungwa kwa Zuma
Lakini Ramaphosa alirithi matatizo na kulazimika kusimamia uchunguzi kuhusu ufisadi uliokithiri serikalini chini ya mtangulizi wake na mkongwe wa chama cha ANC Jacob Zuma.
Wakati huo huo, takwimu za serikali zinaonyesha kuwa raia milioni 18 wanategemea mpango wake wa ruzuku ya kijamii. Idadi ya vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 na 24 ambao hawana kazi ilifikia rekodi ya juu mwishoni mwa mwaka 2021.
Chanzo: DW