Afrika Kusini yakumbuka maandamano ya Soweto
16 Juni 2016"Walijaribu kufanya maandamano, lakini walizuiwa, na waliuawa. Lakini leo hii polisi wako hapa kutusindikiza," alisema kasisi na mkereketwa wa chama cha ukombozi nchini humo, African National Congress ANC, Frank Chikane wakati polisi wawili, mmoja mweusi na mwingine mweupe walipokuwa wakiwasindikiza waandamanaji kuelekea uwanjani.
Machafuko hayo yaliyosababisha kiasi ya watu 170 kuuawa, yalikuwa ni hatua muhimu ya mabadiliko katika harakati za kukabiliana na siasa za ubaguzi wa rangi, kuyaeleza mataifa juu ya utawala wa kikandamizaji, lakini pia yalifungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 1994, ambapo Nelson Mandela, alichaguliwa Rais wa kwanza mwafrika kuongoza nchi hiyo.
Mpiga picha za habari Peter Magubane anasema alinusurika kupigwa risasi ya kichwa wakati akipiga picha za tukio hilo, aliloshuhudia mauaji ya kusikitisha.
"Karibu nipoteze maisha yangu katika mji wa Alexandra tarehe 17 Juni. Risasi ilinipita kichwani ikiwalenga wanawake wawili waliokuwa wanapiga kelele wakisema 'nguvu nguvu'. Nilianguka chini na kuinuka kupiga picha ya mwanamke mmoja wapo aliepigwa risasi tumboni," anasimulia mpiga picha huyo.
Askari waliotumiwa wahudhuria
Wanajeshi wa enzi hizo za ubaguzi, walioajiriwa na Muungano wa majeshi ya Afrika Kusini, SADFA pia walihudhuria maadhimisho haya, wakiwa wamevalia makoti na tai zenye alama za vyeo vya kijeshi vya muungano huo.
"Tunasikitishwa na tukio hili lililotokea miaka 40 iliyopita, na tunaomba msamaha kama bado watu wana maumivu. Lakini huu ni wakati wa kuanza upya, alisema Mwenyekiti wa muungano huo wa kijeshi Jan Malan. "Tunaweza kuomba radhi kwa miaka 100, na haitabadilisha kitu. Tuichukulie miaka hii 40 kama alama na hatua ya kuanza upya kuijenga Afrika Kusini tunayoitaka, alisema.
Takriban watu 400, ambao walikuwa katika makundi ya weupe na weusi walijumuika katika uwanja wa Orlando, uliopo kitongoji cha Soweto kwa ajili ya kumbukumbu hiyo, kabla ya maadhimisho ya kitaifa yanayohudhuriwa na Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, Alhamis hii.
Miongoni mwa wanajeshi wa enzi za ubaguzi, ambao hawakupelekwa kwenye machafuko hayo ya Soweto, walihudhuria kwa mara ya kwanza. Mmoja wa Afisa wa polisi aliyekuwepo kwenye tukio hilo la Soweto alikataa kushiriki.
Muitikio wa wanfunzi uliwashangaza hata waandaji
Dan Montsitsi, aliyekuwa kiongozi wa wanafunzi kwenye tukio hilo, lilitokea June 16, 1976, anasema maandamano hayo yalipangwa kwa muda mrefu. Lakini wazazi hawakujua chochote, hata walimu, na polisi pia hawakujua. "Tulishangazwa na idadi ya wanafunzi waliojitoa kuingia mitaani kupinga agizo hilo la serikali," Montsitsi ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.
Wanafunzi ambao wengi wao walikuwa na sare za shule walibeba mabango ambayo baadhi yaliyosomeka "Kiafrikana kinanuka" na "Kiafrikana kinatakiwa kuondolewa". "Tulikuwa tukiimba na kucheza karibu tu na Orlando West High, na mara ghafla polisi wakaja, hawakuzungumza nasi, na badala yake walitupa dakika tano za kuondoka, na tulipokataa, ndipo walianza kufyatua risasi. Ndani ya siku tatu, idadi kubwa ya watu walikuwa wameuawa."
Wakati huo na sasa!
Montsitsi anasema, Waafrika sasa wanaweza kupiga kura, "lakini mabadiliko nchini mwetu yanakwenda taratibu sana." Mmoja wa vijana ambaye hana ajira Troformo anashindwa kuficha hisia zake na kusema kuna wakati umasikini unaweza kukufanya kufikiria kuna watu walitoa maisha yao bure.
"Tunamalizia safari ambayo wanafunzi wale hawakuimaliza. Amesema, mchungaji Frank Chikane. Mwaka 1976, walibeba mabango yaliyosomeka, "Kiafrikana kinanuka na Kiafrikana kiondolewe", lakini leo hii walionusurika walibeba mabango yenye ujumbe, "Umoja katika tofauti zetu" na "Tusimame wote kama wamoja".
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Idd Ssessanga.