1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

wanajeshi wa Afrika Kusini watuhumiwa kukosa nidhamu DRC

15 Oktoba 2023

Viongozi wa jeshi la Afrika Kusini wamewaamuru wanajeshi wao wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kurudi nyumbani kutokana na kukabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu.

https://p.dw.com/p/4XYe1
Demokratische Republik Kongo | UN Blauhelme nach Kämpfen mit Rebellengruppe M23
Picha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wanajeshi hao kutuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono na maonevu. Wanajeshi hao wataendelea kuwepo nyumbani nchini Afrika Kusini hadi uchunguzi utakapomalizika.

Wanajeshi wa Afrika Kusini wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa
Wanajeshi wa Afrika Kusini wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa MataifaPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Askari hao wanane raia wa Afrika Kusini walikuwa ni sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walikuwa wamezuiliwa kwenye kambi yao katika mji wa mashariki wa Beni mapema mwezi huu.

Jeshi la Ulinzi la Taifa la Afrika Kusini limesema kutokana na uzito wa madai hayo, limechukua uamuzi wa kuwarejesha nchini wanajeshi ili kujibu tuhuma hizo na kutoa maelezo ya matukio yaliyojiri. Jeshi la Afrika Kusini limeongeza kuwa wachunguzi wamepelekwa nchini Kongo kufanya uchunguzi rasmi.

Soma pia:Walinda amani 9 kurejeshwa nyumbani kwa unyayasaji DRC wa kijinsia

Hata hivyo jeshi limesema inasikitisha kwamba serikali ya Afrika Kusini haikuarifiwa moja kwa moja kuhusu madai hayo lakini iliyafahamu kupitia kwenye vyombo vya habari.

Ripoti ya ndani ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeeleza kuwa wanajeshi hao walikiuka pakubwa utaratibu wa sheria za Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane DujarricPicha: Imago/ZUMA Press/M. Brochstein

Mapema wiki iliyopita, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, alisema ujumbe wa amani wa Umoja huo MONUSCO, ulipokea ripoti kwamba wanajeshi wanaodaiwa kuhusika walikuwa wakikutana baada ya saa za amri ya kutotoka nje kwenye baa moja maarufu kwa vitendo vya biashara ya ngono.

Dujarric, amesema maafisa wa polisi wa Umoja wa Mataifa waliokwenda katika majengo hayo kwa ajili ya kutathmini hali na kuwakamata wanajeshi hao, walishambuliwa na kutishiwa na wanajeshi hao wa Afrika Kusini.

Soma pia:Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke DRC

Tangu mwezi Mei, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi amekuwa akitoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, kuiunga mkono nchi hiyo kwa kupeleka walinda amani kwa ajili ya kulisaidia jeshi la Kongo kukabiliana na waasi wa M23, ambao wameyateka maeneo makubwa ya Kaskazini katika jimbo la Kivu.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Lakini serikali hiyo ya mjini Kinshasa pia imekuwa ikitoa wito wa kuharakisha kuondoka kikosi cha Umoja wa Mataifa kuanzia mwezi Desemba, ikikilaumu kwa kushindwa kumaliaza ghasia zinazoendeshwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha kwa muda wa miaka 25 wa kuwepo kikosi hicho kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

Chanzo:AFP