1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yaelekea kuzidiwa na watu

25 Septemba 2018

Idadi ya watu barani Afrika inakuwa kwa kasi ambapo kufikia mwaka 2050 itakuwa imeongezeka maradufu ya ilivyo sasa, huku 40% ya watu masikini kabisa duniani wakihofiwa kuja kuishi kwenye mataifa mawili tu ya bara hilo.

https://p.dw.com/p/35RW4
Spanien | NGO "Proactiva Open Arms"
Picha: Getty Images/AFP/A. Messinis

Kwa sasa barani Afrika wanaishi watu bilioni 1.3. Miaka 32 ijayo, idadi hii itaongezeka mara mbili zaidi, na kama ukuwaji wa kiuchumi hautakwenda sambamba na ukuwaji huu wa idadi ya watu, basi kitakachotokea ni ongezeko la umasikini.

Khofu hiyo imeufanya Wakfu wa mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates, kufanya utafiti wa namna ya kukabiliana na kitisho kijacho. Yaliyogunduliwa na utafiti huo uliopewa jina "Walindamlango 2018" ni kwamba ikifika mwaka 2050, asilimia 40 ya watu walio masikini sana duniani watakuwa wanaishi kwenye mataifa mawili tu: Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hivi sasa, Nigeria inakaliwa na watu milioni 190, ambapo kwa wastani mwanamke mmoja huzaa watoto watano, na hilo lina matokeo yake, kwa mujibu wa Farouk Jega, mkurugenzi wa Wakfu wa Bill na Melinda Gates nchini Nigeria: 

"Tayari hali ni mbaya hapa Nigeria. Umasikini wa kutupwa unazalisha hali ya ukosefu wa usalama, machafuko, uhalifu. Lakini serikali ya Nigeria inajaribu kukabiliana na ongezeko hili la kupindukia la idadi ya watu. Waziri wa afya anapigia kampeni njia za kisasa za uzazi wa mpango. Lakini ni asilimia 10 ya wanawake wanaotumia njia hizo, ambayo ni idadi ndogo. Gharama pia ni kubwa, hasa kwa wanawake na familia za kimasikini," anasema Jega.

Kama ilivyo kwenye mataifa mengine mengi ya Afrika, jukumu la mwanamke nchini Nigeria ni lile lile la kuzaa, kulea watoto na kuhudumia nyumba. Serikali ya Nigeria inapambana kubadili mtazamo huu kwa kushirikiana na asasi za kijamii, viongozi wa kidini na kimila, anasema Faouk Jega, ambaye anaona kuwa kuna aina fulani ya mafanikio kwenye ushirikiano huu. 

Angalau sasa raia wako tayari kujadili faida na hasara za kuwa na watoto wengi na ile mila kwamba mwenye watoto wengi anakuwa amejijengea uhakika wa kuwa na watu wa kumuangalia afikiapo umri wa uzee. Hata hivyo, naye mkurugenzi huyo wa Wakfu wa Bill na Melinda Gates nchini Nigeria, anakiri kuwa: "Panahitajika juhudi kubwa zaidi kubadili imani na mitazamo ya watu."

Elimu kama suluhisho

Njia moja nzuri kabisa kuwezesha hili, ni kutoa elimu zaidi kwa wanawake na kuwapatia vyanzo vya kujipatia kipato, anaamini Farouk Jega, kwani changamoto hizi zapaswa kugeuzwa kuwa fursa. Hata hivyo, hadi sasa idadi ya vizazi haijashuka. Taasisi ya Gates inaona kwamba kutoa elimu ya afya na kuwekeza kwenye elimu ya vijana kutatatuwa tatizo hili kwa ufanisi zaidi. "Ikiwa kila mwanamke barani Afrika angekuwa na uwezo wa kuamua idadi ya watoto awatakao, basi idadi ya watu barani humo ingepungua kwa asilimia 30", unaandika wakfu huo.

Ifikapo mwaka 2050, Nigeria itakuwa na watu zaidi ya milioni 400 na Kongo itakuwa na idadi mara mbili ya ilionao sasa, lakini kwenye mataifa yote mawili, hakuna uhakika ikiwa kutakuwa na chakula cha kutosha wala miundombinu ya kiafya ya kuwahudumia watu hao, anasema Alisa Kaps wa Taasisi ya Idadi ya Watu na Maendeleo ya mjini Berlin, Ujerumani.

"Ongezeko hili la idadi ya watu kwa Kongo na Nigeria ni kubwa mno kwa nchi na haulingani na uwezo wa kuwahudumia. Kawaida ukuwaji wa uchumi unatakiwa kwenda sambamba na ukuwaji wa watu, lakini uchumi na ustawi hauwezi kukuwa kwa kasi moja na watu," anaongeza Alisa Kaps.

Mgongano wa itikadi

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, shughuli za maendeleo zimetanzwa na vita vya kila mara, anasema Frederick Okwayo wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) mjini Johannesburg.

"Hali inazidi kuwa ngumu kwa sababu ya miundombinu mibaya, lakini tunajaribu kufika kwenye makambi ya wakimbizi na kuwasaidia watu, ukiwemo ushauri wa mambo ya familia," anasema Okwayo.

Lakini kwenye suala hili la uzazi, lililo muhimu kwa mataifa takribani yote ya Afrika ni ulazima wa wanaume kushiriki kwa kuuona umuhimu wa kuwa na familia ndogo. Serikali pia zinapaswa kuwa madhubuti kwenye kuongoza mageuzi na kuyasaidia mashirika ya misaada. 

Hapo napo kwenye jukumu la serikali, panakuja suala zima la tafauti za kiitikadi. Bado kuna viongozi barani Afrika ambao hawaamini kabisa suala la kuzuia uzazi.

Hivi karibuni Rais John Magufuli wa Tanzania alinukuliwa akiwashajiisha wanawake kuacha kutumia njia za kuzuia kizazi, kwani taifa hilo lina uhitaji wa watu wengi zaidi.

Kauli hii ni hata katika hali ambapo zaidi ya nusu ya Watanzania milioni 53 wanaishi chini ya mstari wa umasikini, kwa pato la dola mbili kwa siku.

Mwandishi: Martina Schwikowski
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mharir: Mohammed Abdul-Rahman