Ndege ya shirika la Yemen yaangukia bahari ya Hindi
30 Juni 2009Ndege ya abiria ya shirika la Yemenia Air imeangukia katika bahari ya Hindi karibu na pwani ya kisiwa cha Comoro mapema leo.
Watu 153 walikuwemo mnamo ndege hiyo.Mtoto mmoja amenusurika.
Ndege hiyo iliangukia baharini mapema asubuhi leo kiasi cha robo saa kabla ya kuwasili katika kisiwa cha Moroni ambapo ilikuwa inatarajiwa kutua.
Habari zinasema baadhi ya miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo imeonekana. Mashirika ya habari yameripoti kuwa mtu mmoja alienusuruka ameokolewa. Madakatari wamesema kuwa mtu huyo ni mtoto.
Hatahivyo juhudi za uokoaji zinaendelea. Ufaransa imepeleka manowari mbili na ndege moja kutoka kwenye kituo chake cha karibu ili kuisaidia katika juhudi za uokaji.
Ndege ya abiria ya shirika la Yemen aina ya Airbus 310 ilikuwa inatokea Sanaa mji mkuu wa Yemen ikiwa na abiria 142 na wafanyakazi 11. Ilianza safari yake mjini Paris, Ufaransa hapo jana na kutua kwa muda, katika miji ya Marseille,Djibouti na Sanaa.
Mpaka sasa haijabainika kwa uhakika nini hasa kilisababisha ndege hiyo ianguke lakini maafisa wanasema hali ya hewa ilikuwa mbaya wakati yalipotokea maafa.
Ndege hiyo ilijaribu kutua, lakini ilishindikana. Baadae iligeuka na kupaa juu tena na baada ya hapo ilitoweka.
Mkurugenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moroni Hadji Ali alisema hapo awali, kwamba kitengo cha kufuatilia ndege kilipoteza mawasiliano na ndege hiyo ulipobakia muda mfupi kabla ya kutua.
Hatahivyo habari kutoka Paris Ufaransa zinasema kuwa ndege hiyo ilikuwa inamulikwa na idara ya usarifishaji ya Ufaransa kutokana na kugundulika hitilafu nyingi.
Maafisa wa Ufaransa wameeleza kuwa kampuni ya ndege ya Yemen imekuwa inafuatiliwa na idara za Ufaransa na kwamba ndege hiyo iliyoanguka, hapo awali haikuwa inaruka katika anga ya Ufaransa kutokana na hitilafu.
Miongoni mwa abiria, 66 walikuwa wafaransa na watoto watatu wachanga. Lakini idadi kubwa walikuwa wananchi wa Comoro.
Mwandishi:Abdul-Mtullya/AFPE
Mhariri:M.Abdul-Rahman