Ajali ya treni yaua karibu watu 100 India
20 Novemba 2016Maafisa wa polisi wamesema takriban watu 20 bado hawajulikani walipo wakati mamlaka zikijaribu kutafuta chanzo kilichosababisha kuanguka kwa ghafla kwa mabehewa 14 kutoka kwenye reli huko Pukhran kama kilomita 65 kusini mwa mji wa Kanpur wakati treni hiyo ilipokuwa ikisafiri kati ya mji wa kaskazini mashariki wa Patna na mji wa kati wa Indore.
Huku kukiwa na hali ya taharuki na kuchanganyikiwa manusura wamekuwa wakihangaika kuwatafuta ndugu zao na wengine wamekuwa wakijaribu kuingia kwenye mabehewa yalioharibiwa kuwaokowa jamaa zao na kukusanya vitu vyao.
Pratap Rai afisa mwandamizi wa reli amesema wanatumia kila mbinu kunusuru maisha lakini ni vigumu sana kukata mabehewa ya chuma.
Idadi ya vifo kuongezeka
Wakati idadi ya vifo ikitegemewa kuongezeka ajali hiyo inaweza kuwa ajali mbaya kabisa ya reli kuwahi kutokea nchini India tokea mwaka 2005 wakati treni ilipobamizwa na jabali na nyengine kutumbukia mtoni kila moja ikiuwa watu zaidi ya 100.
Mfumo wa reli wa India ulioemewa unashika nafasi ya nne kwa ukubwa duniani ukisafirisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku lakini una rekodi mbaya ya usalama ambapo maelfu ya watu wanakufa katika ajali kila mwaka zikiwemo ajali za mara kwa mara za treni kuacha reli.
Suresh Prabhu waziri wa reli nchini India amesema katika mtandao wa Twitter kwamba serikali itachunguza kwa haraka sababu za treni hiyo kuacha reli na kuahidi uwajibikaji na kuchukuliwa kwa hatua kali.
Mabehewa yaharibiwa vibaya
Mikanda ya video imeonyesha mabebewa yalioharibiwa vibaya huku polisi na watu wakiwa juu ya mabehewa hayo wakitafuta manusura.Maafisa wa uokozi wameonekana wakijipenyeza kwenye umma wa watu huku wengine wakiyaondowa mabehewa yalioinduka kutoka kwenye reli mojawapo ya njia kuu za usafiri wa mizigo na abiria kaskazini mwa India.
Treni hiyo iliokuwa imefurika abiria ambayo huendeshwa na serikali imeacha reli alfajiri ya Jumapili wakati abiria zaidi ya 500 walipokuwa wamelala.Treni kuacha reli na ajali nyengine za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwemo ajali ilitokea Uttar Pradesh jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini India hapo mwezi wa Machi mwaka jana na kuuwa watu 39.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alieanza maisha kwa kuuza chai nje ya vituo vya treni ameahidi kufanya mfumo wa safari za reli nchini India kuwa wa kisasa.
Mwandishi: Mohamed Dahman /Reuters
Mhariri: Zainab Aziz