Akaunti ya Twitter ya Obama, Biden zadukuliwa
16 Julai 2020Mabilionea Bill Gates na Elon Musk ni miongoni pia mwa wahanga wa udukuzi wa akaunti nyingi za Twitter ambao umetokea siku ya Jumatano. Baadhi ya makampuni makubwa kama vile Apple na Uber pia yameangukia katika uhalifu huo uliowalenga watumiaji wa mitandao kwa kutumia sarafu ya mtandaoni ya Bitcoin ili kujipatia fedha.
Ujumbe uliowekwa katika mtandao wa Twitter ambao tayari umefutwa, ulionekana kutoka kwenye akaunti za watu mashuhuri ukiwaeleza watumiaji wa mtandao kwamba wanazo dakika 30 za kutuma kiasi cha dola 1,000 katika akaunti ya Bitcoin ili kujipatia fedha mara mbili.
Akaunti ya Barack Obama, Joe Biden, Kanye West, Jeff Bezos na Mike Bloomberg zilikuwa miongoni mwa akaunti zilizotuma ujumbe huo kutoka kwenye kurasa zao ambazo zimethibitishwa kwa maana ya kwamba zina alama ya tiki ya bluu. Hata hivyo ujumbe huo uliweza kuondolewa baadae.
Soma zaidi Twitter yahakiki ukweli wa ujumbe wa Trump kwa mara ya kwanza
Mtandao wa Twitter umesema kwamba uliondoa ujumbe huo na kuzifunga kwa muda baadhi ya akaunti zilizothibitishwa za watu mashuhuri ili kuzuia uwezekano wa kutuma tena ujumbe wakati wakichunguza tukio hilo.
Kwenye taarifa yake Twitter imesema ''watumiaji huenda wasiweze kutuma ujumbe kwenye akaunti zao ama kubadili nywila wakati tunachunguza na kutoa maelezo ya tukio''.
Kwa kawaidia akaunti zenye uthibitisho katika mitandao ya kijamii ni zile za wanasiasa wa ngazi ya juu ama watu walio na umaarufu katika jamii ikiwemo waandishi habari, wasanii, wakuu wa nchi na taasisi kubwa.
Akaunti bandia ya Bitcoin ambayo inahusishwa na udukuzi huo inasemekana kuwa ilitengenezwa siku ya Jumatano na ilikuwa tayari imepokea karibu sarafu za mtandaoni 12.9 ambazo ni sawa na dola 114,000 hadi kufikia mwisho wa siku. Nusu ya kiasi hicho cha fedha kilifanikiwa kuibwa na wadukuzi.
Wadukuzi walionekana kuwalenga zaidi wanasiasa wa chama cha Democratic au wale wa mrengo wa kushoto na kurejesha kumbukumbu ya kampeni za urais wa Marekani za mwaka 2016. Idara za usalama za Marekani zilithibitisha kwamba Urusi ilitumia mbinu ya udukuzi na mitandao ya kijamii kuingilia uchaguzi. Shirika la Ujasusi la Marekani FBI, limekiri juu ya uhalifu huo, lakini halikutoa maelezo zaidi.
Udukuzi huo pia umedhihirisha usalama hafifu wa mtandao wa Twitter nchini Marekani mnamo wakati taifa hilo linapoelekea kwenye uchaguzi wa rais wa 2020, ambapo mitandao ya kijamii inatazamiwa kuwa na jukumu kubwa. Athari ya tukio hilo zimesababisha wasiwasi miongoni mwa wawekezaji ambapo hisa za Twitter ziliporomoka kwa asilimia tatu.
Chanzo: Mashirika