1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajawazito na watoto mjini Darfur wakabiliwa na utapiamlo

25 Septemba 2024

Wanawake na watoto katika eneo la Darfur Kusini nchini Sudan wanakabiliwa na matatizo makubwa ya afya kuliko mahala pengine popote duniani.

https://p.dw.com/p/4l4jO
Wanawake wakimbizi wa Sudan
Wanawake wakimbizi wa SudanPicha: Mohamed Zakaria//MSF/REUTERS

Wanawake na watoto katika eneo la Darfur Kusini nchini Sudan wanakabiliwa na matatizo makubwa ya afya kuliko mahala pengine popote duniani. Shirika la Madaktari wasio na mpaka, MSF, limesema hali hizo zinahitaji kushughulikiwa kwa haraka na kwamba hali hiyo ni matokeo ya ghasia zinazoikumba nchi hiyo tangu Aprili 2023.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, MSF imesema kwamba vifo 114 vya akina mama wajawazito vilitokea katika kipindi cha kuanzia Januari hadi katikati ya Agosti 2024.

Soma: Wakimbizi wa Sudan wakabiliwa na changamoto kwenye vituo vya kusubiri

Zaidi ya asilimia 50 ya vifo vya akina mama hao wajawazito vilitokea katika mazingira ya matibabu, huku maambukizi yakiwa sababu kuu ya vifo hivyo katika vituo vya afya vinavyosimamiwa na MSF.

Kati ya mwezi Januari na Juni, watoto wachanga 48 walikufa kutokana na maambukizi katika vituo viwili vya afya.

MSF pia imesema utapiamlo miongoni mwa watoto huko Darfur Kusini pia ulizidi viwango vya hali ya dharura na kuongeza kuwa mahitaji ya huduma za matibabu yalizidi kiwango kinachoweza kushughulikiwa na shirika hilo.