1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aleppo yatendewa ukatili - UN

26 Septemba 2016

Umoja wa Mataifa unasema kinachondelea katika mji wa Aleppo ni ukatili usiomithilika, wiki moja baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yakisimamiwa na Urusi na Marekani.

https://p.dw.com/p/2QaMS
Syrien Aleppo Zerstörungen
Moja ya majengo yaliyoharibiwa vibaya na mashambulizi ya anga ya jeshi la Syria katika mji wa kaskazini wa Aleppo.Picha: Picture-Alliance/dpa/Syrian Civil Defense White Helmets

Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza, mashambulizi ya usiku wa jana yaliuwa na kujeruhi watu kadhaa katika mji huo ambao udhibiti wake umegawika nusu kwa nusu kati ya waasi na serikali, wiki moja baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yakisimamiwa na Urusi na Marekani.

Shirika hilo limerikodi vifo 237, wakiwemo watoto 38, ndani ya kipindi cha wiki moja tu. Katika vifo hivyo, 162 vimetokea kwenye eneo la mashariki mwa mji wa Aleppo linaloshikiliwa na waasi. 

"Ni hali ile ile. Hasa nyakati za usiku, mabomu yanaongezeka, yanakuwa mengi zaidi, wanatumia silaha za kila aina, kemikali, mabomu ya kutawanyika. Na sasa angani inapita helikopta, Mungu tu ndiye ajuwaye jengo gani litaangushiwa bomu." Mfanyakazi wa shirika moja la misaada katika upande unaoshikiliwa na waasi, Bebars Mishal, ameliambia shirika la habari la Reuters.

Ukatili wa kutisha 

Jana (25 Septemba), Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa dharura jijini New York kuzungumzia mashambulizi hayo, huku Uingereza, Ufaransa na Marekani zikiitaka Urusi kumdhibiti mshirika wake, yaani serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema kinachoendelea sasa mjini Aleppo ni ukatili uliochupa mipaka na kutoa wito wa kusitishwa haraka kwa mashambulizi dhidi ya raia wasio hatia. 

Ban Ki-moon UN Generalsekretär
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, anasema amechukizwa sana na hali inavyoendelea mjini Aleppo.Picha: REUTERS

"Nimechukizwa sana na kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi katika mji wa Aleppo, ambao umekuwa kitovu kikuu cha kupigwa mabomu tangu kuanza mzozo wa Syria. Matumizi ya mabomu ya kupasulia mahandaki kunaufanya mzozo huu kuingia kwenye kina cha mwisho cha ushenzi. Baraza la Usalama linajadili hali hii, lakini kisingizio gani kinachoweza kuhalalisha kutokuchukuwa hatua za kukomesha janga hili, hadi lini wenye nguvu wataruhusu ukatili huu kuendelea?" Alisema Ki-moon mbele ya waandishi wa habari

Mjumbe wake maalum kwenye mzozo huo, Steffan de Mistura, amesema kamwe hajawahi kushuhudia ukatili unaofanana na kile kinachoendelea sasa nchini Syria, huku akiilaumu jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kuikoa nchi hiyo.

Hata hivyo, mjumbe huyo amesema kwamba dunia haipaswi kukata tamaa na mpango wa Urusi na Marekani kukabiliana na mgogoro huo.

Hayo yanaripotiwa huku taarifa zikisema kwa mara ya kwanza ndani ya miezi sita magari ya misaada ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, yamefanikiwa kuingia katika badhi ya maeneo yenye mzozo usiku wa jana.

Miongoni mwa miji iliyofikiwa na misaada hiyo ni Madaya na Zabadani karibu na mji mkuu, Damascus, na vijiji vya al-Foua na Kefraya kwenye jimbo la Idlib, liliko kaskazini magharibi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf