1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani bila haki ni udikteta, asema kansela Scholz

20 Septemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameonya juu ya suluhu ya maneno matupu, katika kusaka amani nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4WaWF
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz akihutubia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York 19.09.2023.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz akihutubia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York 19.09.2023.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Scholz amesema hayo alipohutubia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Amesema amani bila ya uhuru huwa ni ukandamizaji na amani bila ya haki ni udikteta na kuongeza kuwa Moscow inalazimika kutambua hilo huku akimtolea wito rais Vladimir Putin kumaliza vita vyake nchini Ukraine.

"Lakini vita vya Urusi vimesababisha mateso makubwa sio tu Ukraine. Watu ulimwenguni kote wanateseka kwa sababu ya mfumuko wa bei, ongezeko la madeni, uhaba wa mbolea, njaa na umasikini kuongezeka. Na kwa kuwa vita hivi vina madhara makubwa duniani kote, ni sahihi ulimwengu ushiriki katika kutafuta amani. Wakati huo huo tujihadhari na suluhu za hadaa zinazowakilisha "amani" kwa maneno tu. Amani bila haki ni udikteta. Moscow, pia, lazima ielewe hilo," amesema Scholz.

Kansela Scholz aidha ameunga mkono matamshi ya katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres juu ya umuhimu wa mageuzi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na  huku akisisitiza uwakilishi mpana wa Afrika, Asia na Amerika ya Kusini kwenye baraza hilo.

Soma pia:

Miito ya kumaliza mizozo na uchafuzi wa mazingira yatawala mkutano wa Baraza Kuu

Viongozi wahutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa