Amani ya Sahara Magharibi yanukia
22 Januari 2010Sahara Magharibi inalegalega kati ya ndoto ya amani na kitisho cha vita. Baada ya miaka 35 ya juhudi za kujaribu kuutanzua mojawapo ya mizozo iliyodumu kwa muda mrefu duniani, mkwamo katika mzozo wa Sahara Magharibi unakaribia kuvunjwa. Duru mpya ya mazungumzo kati ya serikali ya Morocco na chama cha Polisario yanapangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Januari au mwanzo wa mwezi ujao wa Februari.
"Tuna matumaini makubwa ya kupatikana suluhu," amesema Bucharaya Beyun, mjumbe wa Uhispania wa chama cha Polisario kinachopigania uhuru wa Sahara Magharibi kutoka kwa Morocco. Wachambuzi nchini Morocco na katika Sahara Magharibi pia wanaona dalili za kupatikana suluhiso la amani katika kuumaliza mzozo huo, ingawa haijabainika wazi juhudi hizo zitaelekea wapi.
Mzozo wa Sahara Magharibi umevuruga uhusiano kati ya Morocco na Algeria inayokiunga mkono chama cha Polisario, hivyo kuongeza hali ya wasiwasi katik eneo hilo, kukwamisha maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano katika kupambana na ugaidi. Umesababisha pia gharama kubwa kwa jumuiya ya kimataifa ambao imetumia mamia ya mamilioni ya dola kuhifadhi tume yake maalum ya kulinda amani huko Sahara Magharibi, MINURSO.
Hata hivyo mzozo wa Sahara Magharibi haujapewa umuhimu mkubwa kiasi cha kuifanya jumuiya ya kimataifa ishinikize kupatikana kwa suluhisho. Hatua hii imesababisha mkwamo ambao unaonekana kuipendelea Morocco. Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani, DPA, mjumbe wa chama cha Polisario nchini Uhispania, Bucharaya Beyun amesema Morocco haitaweza kulazimisha suluhu ambalo halikubaliki na umma wa Sahara Magharibi.
Mzozo wa Sahara Magharibi ulizuka mnamo mwaka 1975 wakati mkoloni wa eneo hilo, Uhispania, ilipoikabidhi Sahara Magharibi kwa Morocco na Mauritania wakati dikteta wa Uhispania Francisco Franco alipokuwa ameaga dunia. Vita vilivyoanzishwa na chama cha Polisario vilichangia pakubwa kuifukuza Mauritania mnamo mwaka 1979 na Morocco ikachukua sehemu yake ya jangwani yenye utajiri wa chumvi ya asidi na uvuvi.
Vita vya miaka 16 vya Polisario dhidi ya Morocco vilimalizika mnamo mwaka 1991 kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano ya Umoja wa Mataifa. Lakini kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sahara haikutekelezwa na Morocco, ambayo inaona kulidhibiti eneo la Sahara Magharibi kuwa mojawapo ya nguzo muhimu za uzalendo wake.
Takriban raia 80,000 wa Sahara Magharibi wanaendelea kuteseka katika kambi za wakimbizi huku wengi kati ya raia wote 200,000 wa eneo hilo wakiwa wakaazi au uzao wa wakaazi wenye haiba ya Morocco. Wajumbe kadhaa wa Umoja wa Mataifa wamejitolea kwa dhati na sasa dola kuu duniani zimeanza kuonyesha kutaka kulifahamu pendekezo jipya lililowasilishwa na Morocco.
Katika pendekezo hilo Morocco inataka Sahara Magharibi iwe na uhuru wa kujitawala lakini isipewe uhuru wake kamili. Swala hilo litajadiliwa kwa kina lakini Morocco inaahidi kuipa Sahara Magharibi uhuru mkubwa wa kujitawala ikiwa ni pamoja na kuwa na bunge lake pamoja na waziri mkuu.
Mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Peter van Walsum, ameuunga mkono mpango huo mpya wa Morocco akiueleza kuwa suluhisho linalofaa. Ufaransa pia inaiunga mkono Morocco lakini Uhispania bado haijatangaza msimamo wake.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Sahara Magharibi Christopher Ross anapanga kujaribu kuanzisha duru mpya ya mazungumzo kati ya Morocco na chama cha Polisario mwishoni mwa mwezi huu wa Januari au mwanzoni mwa mwezi ujao wa Februari mwaka huu.
Mwandishi: Josephat Charo/DPAE
Mhariri: Othman Miraji