1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani yahimizwa Palestina,waisrael wanapoondoka Gaza

9 Agosti 2005

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ahimiza utulivu wakati wa zoezi la waisrael kuondoka Gaza mnamo wiki ijayo

https://p.dw.com/p/CEFV
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ahimiza amani Palestina
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ahimiza amani PalestinaPicha: AP

Huku Mpango wa Ariel Sharon wa kuondoka Gaza ukikaribia,Kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas amewataka Wapalestina kuweka utulivu na vile vile ameahidi kuitisha uchaguzi wa bunge unaosubiriwa kwa hamu mnamo Januari.

Akizungumza na wabunge wa Palestina Abbas amesema kuwepo kwa utulivu upande wa Palestina wakati wa zoezi la waisrael kuondoka Gaza kutaimarisha sifa ya wapalestina machoni mwa walimwengu.

Kiongozi huyo wa wapalestina Mahmoud Abbas aliongeza kusema kuna hitajika hali ya utulivu ili mpango huo uweze kufanikiwa.

Kuwepo amani upande wa palestina kutaunyosha ulimwengu mzima nia yake na ulimwengu utatambua iwapo kweli Palestina inastahili uhuru na kuwa na dola lake.

Eneo la Gaza limekumbwa na mzozo tangu kutangazwa kwa mpango wa kuondoka kwa walowezi wa kiyahudi katika eneo hilo ambao umepangiwa kuanza wiki ijayo.

Serikali ya Israel imepanga kuyavunja makazi 21 ya masetla katika eneo la Gaza pamoja na makazi mengine yaliyoko upande wa magharibi mwa ukanda wa Gaza.

Serikali ya Israel pia imetangaza kuweka wanajeshi wa kuzuia ghasia iwapo wanajeshi au masettla watavamiwa wakati zoezi hilo litakapokuwa likiendelea.

Upande wake rais Mahmoud Abbas ameonya dhidi ya vitendo vya uporaji mali baada ya zoezi hilo akisema ardhi itakayoachwa na masettla ni ya wapalestina wote na haitokuwa mali ya mtu mmoja.

Ametahadharisha pia juu ya kufanywa sherehe nyingi za kusherehekea ushindi huo.

Wakati huo huo mwanadini wa ngazi ya juu wa Palestina ametoa sheria ya kidini dhidi ya tukio lolote la kuuvuruga mpango wa Israel wa kuondoka Gaza.

Mufti huyo pia amesema lazima vitendo vya uporaji mali vikomeshwe wakati zoezi hilo limekamilika.

Kuondoka kwa waisraeli huko Gaza na magharibi mwa ukanda huo kutaadhimisha mara ya kwanza kwa Israel kuwaondosha masettla wakiyahudi katika ardhi ya wapalestina ambayo wameipigania ili kuunda dola lake.

Wapiganaji wakipalestina ambao hadi sasa wangali wanafuata makubaliano yaliyoafikiwa miezi sita iliyopita huko Sharm El Sheikh wanaiona hatua ya Israel kuwa ya ushindi wa kumaliza mzozo huo wa tangu mwaka 2000.

Mahakama ya ulimwengu imeyataja makazi ya masettla wakiyahudi katika maeneo hayo kuwa yasiyo halali lakini Israel inapinga uamuzi huo.

Hata hivyo waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon amesema mpango huo ni kujiondoa katika mzozo na wapalestina.

Uzi Landau kiongozi muasi wa chama cha Likud aliyejaribu kupitia bunge bila mafanikio kuvuruga mpango wa sharon wa kuondoka Gaza amesema kwamba atashiriki katika uchaguzi wa mwanzo kwa tiketi ya chama cha Likud.

Lakini hivi sasa tishio kubwa la mpango huo ni Benjamin Netanyahu aliyejiuzulu kama waziri wa fedha nchini Israel siku ya jumapili.

Lakini kujitumbukiza kwa bwana Landau katika kinyanganyiro cha kutaka uongozi huenda kukaiharibu nafasi ya Netanyahu kwa kuuwagawanya wanachama wenye msimamo mkali katika chama cha Likud.