1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Idadi ya watu walionyongwa iliongezeka mwaka 2022

16 Mei 2023

Kulingana na Amnesty International, idadi ya watu waliouawa kwa kunyongwa ulimwenguni kote mwaka 2022 ilifikia 883.

https://p.dw.com/p/4RQ5m
Symbolbild Galgen
Picha: Nerijus Liobe/Zoonar/picture alliance

Hiyo ni idadi ya juu zaidi ya visa hivyo tangu mwaka 2017, kulingana na  ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International. Ripoti hiyo imeshutumu haswa mashariki ya kati na vilevile kaskazini mwa Afrika.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, ripoti hiyo ya mwaka 2022 inayojumuisha takwimu ya nchi 20 zinazofahamika kwa hukumu ya kuwanyonga watu, ni ongezeko la asilimia 53 la kadhia hiyo ikilinganishwa na mwaka mmoja uliotangulia.

Mtu mwenye uraia pacha wa Iran na Sweden anyongwa nchini Iran kwa hatia ya ugaidi

Ripoti hiyo haijajumuisha kile kinachodaiwa kuwa "maelfu” ya wafungwa ambao huuawa kisiri nchini China. Lakini imejumuisha watu 81 walionyongwa kwa siku moja nchini Saudi Arabia.

Ripoti ya Amnesty International imeeleza kuwa nchi zilizoko Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika mathalan, Iran, Saudi Arabia na Misri, zina hatia ya kuendeleza mauaji ambayo huidhinishwa na serikali.
Ripoti ya Amnesty International imeeleza kuwa nchi zilizoko Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika mathalan, Iran, Saudi Arabia na Misri, zina hatia ya kuendeleza mauaji ambayo huidhinishwa na serikali.Picha: Vincent Yu/AP/picture alliance

Kulingana na ripoti hiyo, China inaaminika kuongoza kwenye visa vya unyongaji, mbele ya Iran iliyowanyonga watu 576, Saudi Arabia iliyowanyonga watu 196, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kwa miaka 30 iliyopita katika historia ya taifa hilo. Misri iliripotiwa kuwanyonga watu 30 na Marekani watu 18.

Iran yathibitisha adhabu ya kifo dhidi ya mtu mwenye uraia wa Iran na Ujerumani

Baadhi ya serikali zinatumia hukumu ya kifo kama silaha ya ukandamizaji

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema matendo hayo yanakiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.Chiara Sangiorgio, mtaalamu wa hukumu ya kifo katika shirika la Amnesty International ameeleza kwamba:

"Katika nchi chache ambazo hukumu hiyo inatumika, tunaona kuna mwendelezo wa juhudi za dola kutumia hukumu hiyo kwa maslahi yake badala ya kutolewa kama adhabu. Wajua baadhi husema hukumu ya kifo huzuia uhalifu, lakini hicho sicho tunachokiona. Zaidi wanatumia adhabu hiyo kuwaadhibu wasio na sauti (na) wapinzani, kama sehemu ya silaha ya ukandamizaji unaofanywa na serikali”.

Japo ukandamizaji rasmi dhidi ya upinzani ni suala lililoongezeka, takriban asilimia 40 ya visa vya unyongaji vilihusishwa na hatia ya ulanguzi au matumizi ya mihadarati, wakiwemo watu 11 waliouawa Singapore.

Wito watolewa wa kutokomezwa kabisa kwa adhabu ya kifo ulimwenguni.
Wito watolewa wa kutokomezwa kabisa kwa adhabu ya kifo ulimwenguni.Picha: Riccardo Antimiani/ANSA/picture alliance

Kwenye ripoti hiyo yake ya kila mwaka, Amnesty International imesema hukumu ya kifo pia hutekelezwa pakubwa nchini Korea Kaskazini na Vietnam, lakini kama ilivyo China, takwimu kamili ni siri kubwa na husalia kugubikwa na giza totoro.

Ripoti: Idadi ya wanaonyongwa Iran yapanda kwa asilimia 25

Agnes Callamard, katibu mkuu wa Amnesty International amesema muda umewadia kwa serikali na Umoja wa Mataifa kuongeza shinikizo dhidi ya wale wanaoendeleza ukiukwaji huo wa haki za binadamu na kuhakikisha ulinzi wa kimataifa umewekwa kwa haki hizo.

Shirika hilo lilieleza matumaini kidogo ya mafanikio kwenye nchi sita ambazo ziliachana na hukumu hiyo mwaka uliopita nazo ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Guinea ya Ikweta, Kazakhstan, Papua New Guinea, Sierra Leone na Zambia.

(Chanzo: AFPE)