1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty Int: Ufalme wa Eswatini uache kukandamiza wakosoaji

20 Oktoba 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limetoa kauli juu ya maandamano yaliyoligubika taifa la Eswatini, na kumtolea mwito mfalme Mswati wa III kuacha ukandamizaji dhidi ya wakosoaji.

https://p.dw.com/p/41uQQ
König Mswati III. von Eswatini
Picha: Gulshan Khan/AFP/Getty Images

Taarifa ya shirika hilo imetolewa siku moja baada ya wabunge wawili Mduduzi Bacede Mabuza na Mthandeni Dube, kufunguliwa mashitaka, tangu walipokamatwa wakati wa maandamano ya mwezi Julai.

Wabunge hao walifunguliwa mashtaka chini ya sehria ya ugaidi pamoja na kukiuka masharti ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Deprose Muchena amesema mamlaka zinatakiwa kuyafuta madai hayo, kwa sababu wabunge hao walikuwa wanatekeleza haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika.

Aidha ameikosoa serikali kwa hatua zake kali dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, lakini pia uamuzi wake wa kuzifunga shule na huduma za intaneti akisema huo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binaadamu.