1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atia saini amri ya kuyaondoa majeshi ya Marekani Syria

24 Desemba 2018

Jeshi la Marekani limesema agizo hilo ni baada ya marais Donald Trump na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kukubaliana juu ya hatua za kuepusha hatari ya kuacha pengo nchini Syria.

https://p.dw.com/p/3Aaim
Argentinien G20 Gipfel - Türkischer Präsident Erdogan und US-Präsident Trump
Picha: picture-alliance/AA/Turkish Presidency/M. Cetinmuhurdar

Uamuzi wa Marekani ambayo imekuwa inashiriki katika kupambana na magaidi wanaojiita dola la Kiislamu IS nchini Syria umewashtua washirika wake duniani kote pamoja na wanasiasa wa nchini Marekani kwenyewe. Msemaji wa jeshi la Marekani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba agizo la kuyaondoa majeshi hayo limetiwa saini, lakini msemaji huyo hakutoa maelezo zaidi.

Uturuki ambayo ni mshirika wa nadra wa Marekani imesifu uamuzi huo ambapo sasa itakuwa na fursa ya kutosha ya kuwalenga wapiganaji wa Kikurdi ambao ni washirika wa Marekani waliotoa mchanngo muhimu katika harakati za kijeshai za kupambana na magaidi hao wanaojiita dola la Kiislamu. Hata hivyo wapiganaji hao wanazingatiwa na Uturuki kuwa magaidi.

Marais Donald Trump na Recep Tayyip Erdogan wamekubaliana baada ya kuzunguma kwa njia ya simu juu ya kuratibisha hatua za kijeshi na kidiplomasia ili kuepuesha pengo nchini Syria baada ya majeshi ya Marekani kuondoka. Lakini wanasiasa wa Marekani na washirika wa Marekani duniani kote wanahofia kuwa hatua ya Marekani imechukuliwa mapema mno.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesikitishwa na uamuzi wa Marekani na amesema kuwa washirika wanapaswa kuaminika. Wakati huohuo, mtaalamu wa masuala ya nje wa chama cha SPD cha nchini Ujerumani Nils Schmidt amesema kuondolewa kwa majeshi ya Marekani kutoka Syria kutatatiza juhudi za kutafuta suluhisho.

Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/abaca

Bwana Schmidt ameeleza kwamba kuondolewa kwa majeshi hayo kutaacha pengo katika muktadha wa vita vya nchini Syria. Ameelezea wasiwasi juu ya nani italitumia pengo hilo? Akizungumza katika mahojiano ya radio mtaalamu huyo wa SPD wa masuala ya nje ametanabahisha kuwa hatua ya Marekani itauacha mgogoro wa Syria utatuliwe na Iran, Uturuki, Urusi na hata Israel.

Hali hiyo itatatiza juhudi za kuutatua mgogoro huo. Mtaalamu huyo amesema Syria imara itakayoweza kuibuka baada ya vita itaweza kujengwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa tu, na ili suluhisho hilo lipatikane Marekani inapaswa kutoa mchango muhimu.       

Wanasiasa kadhaa wa Marekani kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Democtrats wameyapinga madai ya Trump kwamba magaidi wa IS wamechakazwa na badala yake uamuzi huo umesababisha wasiwasi katika jeshi la Marekani kutokana na uwezekano wa Marekani kuwatelekeza washirika wake wa Kikurdi.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo