Angela Merkel bado aongoza hana mpinzani
24 Novemba 2017Miaka kumi na mbili iliyopita kansela Angela Merkel aliibuka kuwa kansela wa kwanza mwanamke nchini Ujerumani. Na hadi sasa kama kusingetokea matatizo katika kuunda serikali ya umoja baada ya kumalizika uchaguzi bibi Merkel angelikuwa ni kansela aliyechaguliwa kwa mara ya nne lakini baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja na vyama vingine bibi Merkel anakosa wingi wa viti ndani ya bunge la Ujerumani "Bundestag”.
Hali hii naweza kuonekana kana kwamba mgogoro unanukia au nguvu ya Merkel inapungua. Lakini wala haionyeshi hali kuwa imefikia mahala hapo hasa wakati bibi Merkel pale alipotembea ndani ya bunge, na kupena mikono na wabunge. Na mara alipomuona na kumpungia mkono Paul Ziemiak, mwenyekiti wa tawi la vijana la chama chake cha CDU na baadae wawili hao wakaketi pamoja nyuma ambako kulikuwa hakuna watu na wakafanya mazungumzo ya faragha.
Ziemiak na wafuasi wake mara nyingi katika siku zilizopita walikuwa wakimlaumu Kansela Angela Merkel lakini kwa sasa wanaonekana kuwa wamebadili mawazo yao na kuunga mkono kauli zinazoashiria kuwa bibi Merkel ndiye chaguo zuri katika kuiongoza nchi: anasema "Ujerumani inahitaji utulivu, na kama kuna mtu anayesimama utulivu, basi mtu huyo ni Angela Merkel. "
Lakini maneno hayo siyo waliyokuwa wakiyasema siku za hivi karibuni baada ya uchaguzi wa Septemba 24.Chama cha Christian Democtarac Union (CDU) pamoja na chama ndugu cha Christian Social Union (CSU) vyama hivyo vilipata asilimia 33 tu ya kura,hayo yakiwa ni matokeo yao mabaya kabisa tangu 1949.
Kutokana na kitisho hicho cha kupoteza umaarufu tawi la vijana wa CDU lilisema kuwa chama hicho kimepoteza uaminifu wake. Vijana wa tawi la CDU walisema ahadi kuu katika uchaguzi ya muendelezo na utulivu, haitoweza tena kutekelezwa. Lakini Kansela haoni sababu yoyote ya kujilaumu kwa kushindwa kwenye uchaguzi.
Andreas Rinke, mwandishi wa habari na shirika la habari la Reuters ambaye yuko mjini Berlin mesema Merkel anaona mambo tofauti kabisa na taswira iliyopo, yaani kwa mtazamo wake anaona kuwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa si mazuri lakini sio mabaya. mwandishi huyo amekuwa akifuatilia hatua za Merkel kwa miaka mingi na mnamo mwaka 2016 alitoa kitabu kinacho muhusu kansela Merkel : "Das Merkel-Lexikon: Die Kanzlerin von A-Z" yaani ufafanuzi wa Merkel kuhusu Ukansela kutoka A mpaka Z.
Katika kitabu hicho cha Rinke, neno "kushindwa" lina sehemu yake kwenye ukurasa na mwisho wake kuna mstari unaosema: "Kwa Merkel, kushindwa si sawa na kushindwa kabisa na wa mwisho."
Kuvunjika kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa mwishoni mwa wiki na bila shaka huko ni kushindwa amesema Rinke. Kwa wiki zaidi ya nne, Kansela Merkel alijaribu kuunda ushirikiano na chama cha watetea mazingira cha Kijani na chama cha Waliberali cha FDP lakini alishindwa. FDP ilitoka kwenye mazungumzo hayo na kuelekeza lawama kwa bibi Merkel.
Lakini badala ya kumlaumu Merkel, wanachama wa chama chake walimshukuru na kumpa sifa na wakaonyesha kuendelea kumuunga mkono. Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi, huku klikuwa ni kushindwa kwa mara ya pili, lakini hata hivyo, ushirikiano wa vyama vya CDU-CSU unabakia imaranyuma ya kansela Merkel. Mwandishi Rinke anasema "Siasa wakati mwingine husababisha hali ya kimafumbo yaani ijapokuwa jambo ni sahihi lakini huonekana kama sio sahihi na hivyo kumuweka mtu katika njia panda.
Haijafahamika jinsi Angela Merkel atakavyojinasua kwenye hali ngumu ya sasa. Je, yeye atafaulu kuyafufua mazungumzo yaliyovunjika na hatimaye kuunda serikali ya mseto na vyama vigdogo vya Kijani na FDP, au atatafuta tena ushirikiano na chama kikuu cha upinzani cha Social Democratic SPD? au ataamua kuitisha uchaguzi mpya?
Jambo moja la uhakikani kwamba Merkel atabaki kuwa kansela wa Ujerumani. Katika mahojiano wiki hii, bibi Merkel amesema yuko tayari kutumikia kwa miaka mingine minne ijayo - hata ikiwa uchaguzi mpya utafanyika. Kuhusu hali ya kutatanisha inayomkabili kwa sasa jibu lake lilikuwa. "Kwa kweli, mimi siogopi kitu chochote,".
Mwandishi: Zainab Aziz/dw.com/p/2oAHC
Mhariri: Mohammed Khelef