Annan aelezea matumaini juu ya mkutano wa Syria
29 Juni 2012Kikwazo kikubwa kwa mkutano huo ni msimamo wa Urusi kusisitiza mabadiliko yafanywe katika mpango wa Kofi Annan, ambao unataka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Syria, ambayo itashirikisha wajumbe kutoka upande wa serikali na ule wa waasi.
Hata hivyo mpango huo uneeleza kuwa wajumbe watakaokubaliwa kutoka upande wa serikali, ni wale ambao kushiriki kwao hakuwezi kukwamisha mchakato wa kuleta utengamano na maridhiano.
Wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi, wamemueleza Kofi Annan kuwa mkutano huo wa Jumamosi mjini Geneva hautakuwa na maana yoyote, hadi pale maafikiano yatakapofikiwa baina ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov ambao watakutana leo jioni mjini Petersburg, Urusi.
Urusi yataka marekebisho
Urusi, kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje, inasema mkutano wa Geneva unapaswa kuunga mkono mazungumzo baina ya wasyria wenyewe, bila kuamua juu ya mada ya mazungumzo hayo.
''Mkutano wa Mjini Geneva hauna budi kuunga mkono mpango wa amani wa Kofi Annan. Unapaswa kuweka mashariti ya kumalizika kwa ghasia nchini Syria, na kuanza kwa mjadala unaozihusisha pande zote nchini Syria. Lakini haupaswi kuamua juu ya maswala yatakayozungumziwa.'' Amesema Lavrov.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Urusi, Mkutano baina ya Bi Clinton na Lavrov utakuwa mgumu, kwa sababu unafanyika wakati nchi zao zikitupiana lawama za kusisaidia kijeshi pande tofauti katika mgogoro wa Syria.
Mawaziri wengine wa mambo ya nchi za nje watakaoshiriki katika mkutano huo ni kutoka Uingereza, Ufaransa, China, Kuweit, Qatar na Uturuki, na kuhudhuria kwao kunalenga kuonyesha jinsi nchi hizo zinavyounga mkono mpango wa Kofi Annan.
Assad kutengwa
Wanadiplomasia wanasema kuwepo kwa masharti juu ya maafisa wa serikali ambao kwa mujibu wa mpango wa Kofi Annan wanafaa kushirikishwa katika serikali ya umoja wa kitaifa, kunamaanisha kuwa rais Bashar al Assad hataruhusiwa kushiriki katika serikali, ingawa hilo halielezwi wazi wazi. Wanadiplomasia hao wamesema kuwa vigezo hivyo hivyo vinaweza kuwaengua wajumbe kutoka upande wa upinzani.
Licha ya changamoto hizo lakini, Kofi Annan amesema leo kuwa bado anayo matumaini kuwa mkutano huo utafanyika na utakuwa na matokeo ya kuridhisha. Msemaji wake Ahmad Fawzi amewaambia waandishi wa habari kuwa maandalizi ya mkutano huo yanaendelea kama kawaida.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman