Annan alitaka baraza la usalama kuondoa mkwamo
17 Machi 2012Akihutubia kikao cha faragha cha baraza hilo lenye wajumbe 15 kwa njia ya video , Annan amesema ikiwa kutakuwa na uungwaji mkono imara kwa juhudi zake za kupatanisha ili kufikia kusitishwa kwa mapigano , nafasi itakuwa kubwa zaidi kwake kuweza kumaliza kabisa mapigano. Ujumbe utakaokuwa na nguvu zaidi na umoja , utakuwa ni nafasi nzuri ya kuweza kubadilisha mwelekeo wa mzozo huu, amesema mjumbe katika baraza hilo , akitoa muhtasari wa maelezo ya Annan .
Annan ameeleza kuwa majibu ya Syria kuhusiana na mapendekezo yake ya amani yenye vipekee sita yanavunja moja hadi sasa , lakini kikosi chake bado kinazungumza na serikali ya Syria, amesema mwanadiploamsia huyo.
Annan anahimiza kupatikana usitishaji wa mapigano, upelekaji wa waangalizi na mazungumzo ya kisiasa kati ya serikali na upinzani.
Annan pia amesema katika ujumbe wake kuwa mbinyo wenye mwelekeo wa pamoja ambao umekuwa ukitolewa na baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya Syria umefanikiwa hapo kabla , kama vile kuilazimisha serikali ya Syria kuondoa majeshi yake kutoka nchi jirani ya Lebanon. Kuondolewa kwa majeshi hayo kulikamilika mwaka 2005.
Urusi na China mara mbili zimepiga kura ya turufu dhidi ya maazimio ya baraza hilo yanayoishutumu serikali ya rais Bashar al-Assad nchini Syria, kwa juhudi zake zilizodumu mwaka mmoja sasa kuuzima uasi unaodai demokrasia nchini humo. Umoja wa mataifa unasema kuwa mashambulio ya majeshi ya Assad dhidi ya waandamanaji yamesababisha watu zaidi ya 8,000 wengi wao raia kuuwawa.
Majadiliano juu ya mswada wa tatu wa azimio , mara hii ukiandikwa na Marekani na unaotoa wito wa kusitishwa mapigano na kupata nafasi kwa mashirika ya kutoa misaada kupeleka misaada ya kiutu, umekwama kuhusiana na makubaliano juu ya nani nchini Syria kwanza asitishe mapigano na nani alaumiwe kwa kuzusha mzozo huo.
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva baada ya kutoa maelezo hayo, Annan amesema , "Nina matumaini hivi karibuni kuwa mtasikia sauti moja katika baraza la usalama."
Balozi wa Syria katika umoja wa mataifa , Bashar Ja'afari, amewaambia waandishi habari kuwa kikosi cha ufundi kutoka katika ofisi ya Anna kitawasili mjini Damascus Jumapili. Msemaji wa Annan , Ahmad Fawzi , amesema kuwa watajadili wazo la kupeleka wachunguzi wa kimataifa nchini Syria.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Amina Abubakar