Annan amelihutubia bunge la Kenya hii leo
12 Februari 2008Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amelihutubia bunge la Kenya hii leo kuhusu mazungumzo ya upatanisho yanayoonekana kuwa matumaini bora kurejesha uthabiti nchini humo kufuatia machafuko yaliyosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana.
Annan amesema hakuna haja ya kuhesabu kura lakini akapendekeza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Aidha kiongozi huyo amependekeza kuundwe serikali ya mseto.
Wajumbe wanaomuwakilisha rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekubaliana juu ya kuyamaliza machafuko na kukabiliana na janga la kibinadamu lililoikumba nchi hiyo.
Hata hivyo viongozi hao bado wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kufikia suluhisho la kuumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo kati ya serikali na upinzani.
Kofi Annan na wajumbe wa pande zote mbili wameondoka mjini Nairobi kwenda mahali pasipojulikana ili kuendelea na mazungumzo ya dharura. Amewataka wajumbe wafikie makubaliano katika muda wa siku mbili hadi tatu zijazo.
Wakati huo huo rais Mwai Kibaki ametangaza rasmi mpango utakaotoa elimu ya bure katika shule za sekondari na kuahidi kuwasaidia wanafunzi waliolazimika kuyakimbia makazi yao wakati wa machafuko warudi shuleni.
Akitimiza ahadi yake ya kampeni rais Kibaki amesema serikali yake itatoa dola milioni 42 kwa awamu ya kwanza ya mpango huo, unaotarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi kufikia milioni 1.4.
Rais Kibaki alitangaza elimu ya bure katika shule za msingi wakati wa awamu yake ya kwanza madarakani.