1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan aona uwezekano wa mpango wa amani kutekelezwa

11 Aprili 2012

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu nchini Syria, Kofi Annan, leo amesema kwamba bado yapo matumaini kwamba mpango wa amani wa Syria utafuatwa.

https://p.dw.com/p/14bSr
Kofi Annan na Ali Akbar Salehi
Kofi Annan na Ali Akbar SalehiPicha: ISNA

Annan alisema hayo alipokuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo huko Tehran, mji mkuu wa Iran. Akiwa mwenye matumaini juu ya kufanikiwa kwa mpango wa amani wa Syria, Annan alisema kwamba hali ya usalama nchini humo itaweza kuboreshwa hadi kufikia kesho saa 12 asubuhi, iwapo pande mbili zinazopigana zikiamua kuuheshimu mpango alioupendekeza. "Bado tunao muda kati ya sasa hadi kesho tarehe 12 kusimamisha mapigano," alisema Annan. "Ninaziomba pande zote kuhusika: kwanza kabisa serikali na vile vile waasi." Kwa mtazamo wa Annan, wazo la Qatar na Saudi Arabia, la kuwapa silaha waasi wa Syria, litaifanya hali nchini humo kuwa mbaya zaidi.

Ziara ya Annan nchini Iran inatazamwa kama ni wito kwa taifa hilo la kiislamu kuutumia ushawishi wake ili kuwezesha kumalizika kwa mgogoro nchini Syria. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Bw. Ali Akbar Salehi, katika mkutano na waandishi wa habari alisema kwamba Iran itaendelea kuuunga mkono mpango wa amani alioupendekeza Annan.

Mkutano wa nchi za G8 kujadili kuhusu Syria

Mataifa makubwa yameonyesha wasiwasi juu ya kutekelezwa kwa mpango wa amani wa Syria. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi zenye nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi, zinazounda kundi la G8, leo watakutanana mjini Washington, Marekani kujadili kwa kina kuhusu Syria. Mawaziri kutoka nchi hizo nane ambazo ni Marekani, Urusi, Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italy na Japan watazungumzia pia mpango wa Korea ya Kaskazini wa kurusha roketi angani. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, jana alisema kwamba katika mkutano huo, takaofanyika kwa siku mbili, atazungumza zaidi na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, kuhusu mpango wa amani wa Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: dapd

Wakati huo huo mapigano yameendelea kuripotiwa leo katika baadhi ya maeneo ya Syria. Wanajeshi wa nchi hiyo waliushambulia kwa risasi mji wa Homs na kufanya msako katika eneo la kusini la mji huo. Shirika linalotetea haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake makuu Uingereza, limeeleza kwamba vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad viliuvamia pia mkoa wa Daraa ambao umekuwa ngome kuu ya wapiganaji wa upande wa upinzani.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman