Annan ayataka mataifa ya Afrika kujenga usalama wa chakula.
9 Desemba 2007Lisbon. Katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan ametoa wito wa kuwa na mageuzi ya kijani yanayohusu ushirikiano baina ya serikali za mataifa ya Afrika na wakulima ili kuondoa tatizo la njaa katika bara hilo masikini zaidi duniani.
Amesema lengo ni kuongeza kwa mara tatu uwezo wa usalama wa chakula katika muda wa miaka mitano. Annan ameyasema hayo pembezoni mwa mkutano wa mataifa ya Afrika na umoja wa Ulaya mjini Lisbon. Mapema jana Jumamosi , waziri mkuu wa Hispania Jose Luis Zapatero ametoa wito wa kupatikana mkataba kati ya mataifa ya Afrika na umoja wa Ulaya wa kupambana na uhamiaji haramu. Zapatero amewaambia viongozi katika mkutano huo kuwa mkataba wa aina hiyo utaimarisha elimu, ajira na miundo mbinu katika nchi za Afrika. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel , katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo , amesema rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anachafua heba ya bara la Afrika. Merkel ametoa wito kwa viongozi kupigania demokrasia nchini Zimbabwe. Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesusia mkutano huo kwasababu ya kuhudhuria Mugabe.